Wamagharibi: Uwezekano wa kuzuka Vita vya Tatu vya Dunia ni mkubwa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i23032-wamagharibi_uwezekano_wa_kuzuka_vita_vya_tatu_vya_dunia_ni_mkubwa
Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa kwenye nchi za Magharibi unaonesha kuwa, watu wengi wa nchi hizo wanaamini kwamba Vita vya Tatu vya Dunia vimekaribia na kwamba mapigano makali ya pande zote yanaijongelea dunia hivi sasa.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Jan 07, 2017 23:42 UTC
  • Wamagharibi: Uwezekano wa kuzuka Vita vya Tatu vya Dunia ni mkubwa

Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa kwenye nchi za Magharibi unaonesha kuwa, watu wengi wa nchi hizo wanaamini kwamba Vita vya Tatu vya Dunia vimekaribia na kwamba mapigano makali ya pande zote yanaijongelea dunia hivi sasa.

Televisheni ya Press TV imelinukuu gazeti la Independent la nchini Uingereza likichapisha matokeo hayo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na taasisi maarufu ya YouGov na kusambazwa jana Jumamosi.

Uchunguzi huo umefanyika kwa kuulizwa maswali mbalimbali watu elfu 9 kutoka nchi tisa tofauti za Magharibi. Kwa mujibu wa uchunguzi huo wa maoni, wananchi wa Marekani wanaamini kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa kutokea Vita vya Tatu vya Dunia.

Nusu ya Waingereza wanaamini kuna uwezekano wa kutokea Vita vya Tatu vya Dunia 

 

Mtazamo huo wameuonesha pia wananchi wa Ufaransa, Ujerumaini na Uingereza. Karibu asilimia 64 ya Wamarekani wanaamini kuwa ulimwengu umekaribia kuingia kwenye vita vikubwa huku asilimia 15 tu ya Wamarekani wakiamini kuwa dunia inaelekea kwenye usalama na amani.

Uchunguzi huo wa maoni umeonesha pia kwamba asilimia 19 ya wananchi wa Uingereza wanaamini kuwa upo uwezekano wa kurejea amani duniani lakini asilimia 61 ya wananchi hao wamesema, kuna uwezekano wa kutokea vita vikubwa vya pande zote ulimwenguni.

Hata hivyo wananchi wa nchi za Scandanavia yaani kaskazini mwa Bara Ulaya wakiwemo wa Sweden, Finland na Norway wameonesha hamu ndogo sana ya kuamini kuwa dunia imekaribia kutumbukia kwenye vita vikubwa.

 

Uchunguzi huo wa maoni umeonesha pia kuwa, sababu iliyowafanya wananchi wengi wa nchi za Magharibi waamini kuwa ni jambo lililo mbali kupatikana amani na usalama duniani ni kuweko mapigano makali nchini Syria na kuwepo genge la kigaidi la Daesh katika eneo la Mashariki ya Kati na mlolongo wa mashambulizi ya kigaidi katika kona mbalimbali za dunia na pia matamshi ya kuchochea chuki ya Donald Trump, rais mteule wa Marekani.