Indonesia: Tumeshangazwa na jeshi la Sudan kuwatia mbaroni askari wetu
Serikali ya Indonesia imetangaza kuwa, imeshangazwa na hatua ya jeshi la Sudan kuwatia mbaroni askari wa nchi hiyo na kwamba, kitendo hicho ni kinyume na sheria.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Indonesia imesema kuwa, Jakarta imeanzisha uchunguzi kuhusiana na hatua hiyo ya kutiwa nguvuni askari wake wanaosimamia amani nchini Sudan na kutuhumiwa kuwa wamefanya magendo ya silaha.
Mwanzoni mwa wiki hii vyombo vya habari vya Sudan viliripoti habari ya kutiwa mbaroni maafisa kadhaa wa askari polisi wa Indonesia katika jimbo la Darfur kaskazini, magharibi mwa Sudan.
Askari hao waliohudumu kwa kipindi cha mwaka mmoja katika operesheni ya askari wa Umoja wa Mataifa wa kusimamia amani nchini humo, walitiwa mbaroni wakati walipokuwa wanarejea nchini kwao. Inaelezwa kuwa, silaha kadhaa zilinaswa katika mifuko ya askari hao wa kusimamia amani ambao wamezuiliwa kutoka Darfur kuendelea na safari yao.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Indonesia imelaani kitendo hicho na kutangaza kwamba ripoti ilizotolewa na serikali ya Sudan kuhusiana na tukio hilo imepotoshwa.