Jaji nchini Marekani azuia kutekelezwa nchi nzima marufuku iliyowekwa na Trump
https://parstoday.ir/sw/news/world-i24675-jaji_nchini_marekani_azuia_kutekelezwa_nchi_nzima_marufuku_iliyowekwa_na_trump
Jaji wa Mahakama ya Federali katika wilaya ya Seattle jimboni Washington nchini Marekani ametoa amri ya muda ya kusimamishwa nchi nzima utekelezaji wa marufuku yenye utata ya kuingia nchini humo iliyowekwa na rais Donald Trump dhidi ya raia wa nchi saba za Kiislamu, japokuwa tayari serikali yake imetangaza kuwa itakata rufaa ya dharura dhidi ya uamuzi huo kupitia idara yake ya sheria.
(last modified 2026-04-28T05:09:17+00:00 )
Feb 04, 2017 04:03 UTC
  • Jaji nchini Marekani azuia kutekelezwa nchi nzima marufuku iliyowekwa na Trump

Jaji wa Mahakama ya Federali katika wilaya ya Seattle jimboni Washington nchini Marekani ametoa amri ya muda ya kusimamishwa nchi nzima utekelezaji wa marufuku yenye utata ya kuingia nchini humo iliyowekwa na rais Donald Trump dhidi ya raia wa nchi saba za Kiislamu, japokuwa tayari serikali yake imetangaza kuwa itakata rufaa ya dharura dhidi ya uamuzi huo kupitia idara yake ya sheria.

Amri hiyo iliyotangazwa na Jaji James Robart ni ya uga mpana zaidi kulinganisha na nyingine zinazofanana nayo ambazo zimetangazwa hapo kabla na imetoa pigo kubwa zaidi kwa hatua iliyochukuliwa na Trump.

Saa kadhaa baada ya kutangazwa amri hiyo, mamlaka za Forodha na Mipaka za Marekani ziliyataarifu mashirika ya ndege kuwa yanaweza kusafirisha abiria waliokuwa wameathiriwa na marufuku iliyowekwa na Rais wa nchi hiyo.

Rais Donald Trump wa Marekani

Uamuzi wa Jaji Robart umetangazwa baada ya Mwanasheria Mkuu wa jimbo la Washington Bob Ferguson kufungua shauri la kisheria la kutaka kubatilishwa vifungu vikuu vya amri ya Trump ya kuwapiga marufuku raia wa nchi saba za Kiislamu kuingia nchini Marekani.

Akizungumza mara baada ya kutolewa amri hiyo, Ferguson amesema uamuzi wa jaji Robart ni wa kihistoria na umeonesha kuwa hakuna aliye juu ya sharia, hata akiwa ni rais.

Jaji James Robart

Tarehe 27 ya mwezi uliopita wa Januari rais wa Marekani alitoa amri ya kupiga marufuku kuingia nchini humo katika kipindi cha siku 90 raia kutoka Iran, Iraq, Syria, Yemen, Sudan, Libya na Somalia. Amri hiyo aidha inawazuia wakimbizi kutoka Syria kuingia Marekani kwa muda usiojulikana na vilevile imesimamisha utoaji vibali vyote vya kuingia wakimbizi nchini humo kwa muda wa siku 120…/