UNHCR yaonyesha wasiwasi kuhusu sheria mpya za Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i26104-unhcr_yaonyesha_wasiwasi_kuhusu_sheria_mpya_za_marekani
Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR Filippo Grandi ameeleza wasiwasi wake juu ya dikrii ya rais Donald Trump wa Marekani kuhusu raia wa nchi sita za Kiislamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 08, 2017 12:37 UTC
  • UNHCR yaonyesha wasiwasi kuhusu sheria mpya za Marekani

Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR Filippo Grandi ameeleza wasiwasi wake juu ya dikrii ya rais Donald Trump wa Marekani kuhusu raia wa nchi sita za Kiislamu.

Grandi amesema kufuatia kusainiwa kwa amri hiyo, UNHCR inasisitiza tena kuwa wakimbizi ni watu wa kawaida waliolazimika kukimbia vita, vurugu na mateso katika nchi zao, wenye mahitaji ya msaada wa haraka na ulinzi. Shirika hilo limesema liko tayari kushirikiana kiujenzi na serikali ya Marekani kuhakikisha mipango yote ya wakimbizi inafikia viwango vya juu vya usalama.

Baada ya siku kadhaa za gumzo na mijadala, hatimaye siku ya Jumatatu Trump alitia saini dikrii mpya ya kuwazuia raia wa nchi sita za Kiislamu kuingia nchini humo.

Maandamano ya kupinga dikrii ya Trump ya kuwapiga marufuku Waislamu kuingia Marekani

Kwa mujibu wa dikrii hiyo mpya, raia wa nchi hizo za Kiislamua ambazo ni Iran, Syria, Yemen, Somalia, Sudan na Libya watapigwa marufuku kuingia Marekani kwa muda wa siku 90 zijazo. Serikali ya Marekani imedai kuwa hatua hiyo imechukuliwa ili kuimarisha usalama na kuzuia eti magaidi kuingia nchini humo.

Mahakama ya Federali ya Marekani ilikataa kutekeleza dikirii ya kwanza ya Trump  ya kuwazuia raia wa nchi saba kuingia Marekani na kuitaja dikrii hiyo kuwa ya kibaguzi. Lakini sababu ambazo zilipekekea mahakama kupinga amri ya Trump bado zipo.