Korea Kusini yadai kuwa, Korea Kaskazini imemtusi rais wao
Jeshi la Korea Kusini limeituhumu Korea Kaskazini kwa kutuma vipeperushi inavyodai kuwa, vimemvunjia heshima Rais Park Geun-hye wa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa jana Jumatano na jeshi la Korea Kusini imesema kuwa, serikali ya Pyongyang imesambaza vipeperushi hivyo katika mji wa Paju unaopatikana katika mkoa wa Gyeonggi-do na kwamba imemvunjia heshima Rais Park Geun-hye wa nchi hiyo. Jeshi hilo limeongeza kuwa, karibu vipeperushi 1000 vimesambazwa na polisi wa Korea Kaskazini katika mji huo na kwamba kuna uwezekano hatua hiyo imechukuliwa kama radiamali kufuatia maneva ya kijeshi ya pamoja kati ya Korea Kusini na Marekani. Itakumbukwa kuwa Jumapili iliyopita, serikali ya Korea Kaskazini iliitishia Korea Kusini na Marekani kwamba hazitakuwa katika amani ya mashambulizi ya nyuklia endapo zitafanya manuva ya kijeshi ya pamoja. Katika radiamali yake juu ya vikwazo vikali vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi yake, kufuatia majaribio yake ya bomu la Hydrogen na pia kurusha kombora la kubebea satalaiti, wiki iliyopita kiongozi wa Korea Kaskazini alitoa amri kwa jeshi la nchi yake kujiweka tayari kwa ajili ya kutumia silaha za nyuklia dhidi ya adui.