The Guardian: Hakuna anayeweza kudhibiti tabia za kimabavu za Trump
https://parstoday.ir/sw/news/world-i27784-the_guardian_hakuna_anayeweza_kudhibiti_tabia_za_kimabavu_za_trump
Gazeti la The Guradian linalochapishwa Uingereza limekosoa shambulio la kombora la Marekani dhidi ya Syria na udondoshaji wake wa bomu la 'mama wa mabomu yote' nchini Afghanistan na kusisitiza kuwa "hakuna mtu awezaye kumdhibiti Rais Donald Trump wa Marekani."
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 14, 2017 22:00 UTC
  • The Guardian: Hakuna anayeweza kudhibiti tabia za kimabavu za Trump

Gazeti la The Guradian linalochapishwa Uingereza limekosoa shambulio la kombora la Marekani dhidi ya Syria na udondoshaji wake wa bomu la 'mama wa mabomu yote' nchini Afghanistan na kusisitiza kuwa "hakuna mtu awezaye kumdhibiti Rais Donald Trump wa Marekani."

Katika makala iliyoandikwa na Simon Jenkins katika toleo la jana Ijumaa la gazeti hilo, mwandishi huyo ameashiria nafasi ya mabomu likiwa ni chombo cha gharama kubwa, angamizi na cha kistratijia kilichoko mikononi mwa wanasiasa na kueleza kwamba, katika miaka 16 iliyopita hadi sasa, Marekani na Uingereza zimeafikiana kuzishambulia kijeshi nchi za Waislamu zisizo na uthabiti; na mashambulio hayo hayajawa na matokeo mengine isipokuwa kusababisha vifo na mchafukoge.

Simom Jenkins

Jenkins ameongeza kuwa katika muda wa wiki moja iliyopita, Donald Trump, kinyume na ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi kuhusu upinzani wake dhidi ya kujiingiza kijeshi nje ya nchi, amezishambulia kijeshi Syria na Afghanistan; na hii ni pamoja na kwamba nchi hizo haziko katika hali ya kutishia usalama wa taifa wa Marekani.

Bomu la mama wa mabomu yote

Mwandishi huyo wa gazeti la The Guardian amefafanua katika makala yake hiyo kwamba majeshi ya nchi za Magharibi yameonyesha wazi kuwa yamechoshwa na vita vya ardhini visivyo na tija katika maeneo ya mbali ya dunia, na kwa hivyo kazi hiyo sasa inafanywa na ndege zisizo na rubani za droni, makombora ya 'cruise' na 'mama wa mabomu yote' ambapo kuwashambulia na kuwaua kimakosa raia katika mji wa Mosul nchini Iraq ni sehemu ya hasara na maafa yanayosababishwa na mbinu hiyo ya kivita.

Simon Jenkins ameeleza kuwa ni wazi kwamba Marekani inaongozwa na mtu ambaye waungaji mkono wake wanakabiliwa na changamoto kwa ajili ya kumdhibiti.../