Noam Chomsky: Trump amevaa mkanda wa kuiangamiza dunia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i28426-noam_chomsky_trump_amevaa_mkanda_wa_kuiangamiza_dunia
Noam Chomsky, mwanafalsafa na mtaalamu mkubwa wa lugha nchini Marekani amesema kuwa, serikali ya Rais Donald Trump imekusudia kwa dhati kuiangamiza dunia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 29, 2017 22:00 UTC
  • Noam Chomsky: Trump amevaa mkanda wa kuiangamiza dunia

Noam Chomsky, mwanafalsafa na mtaalamu mkubwa wa lugha nchini Marekani amesema kuwa, serikali ya Rais Donald Trump imekusudia kwa dhati kuiangamiza dunia.

Chomsky ameyasema hayo katika mahojiano ya kipindi cha televisheni cha ' Democracy Now!' ambapo kwa mara nyingine tena ameashiria matamshi yake ya mwezi Novemba mwaka jana aliyoyatoa kuhusiana na chama cha Republican cha Rais Donald Trump na kusema kuwa, chama hicho ni "taasisi hatari sana katika historia ya mwanadamu." 

Noam Chomsky, mwanafalsafa na mtaalamu mkubwa wa lugha nchini Marekani 

Ameongeza kuwa, serikali ya Trump imeonyesha kwamba, haiupi umuhimu wowote mustakbali wa dunia na imekusudia kwa dhati kuondoa mfumo ambao utasaidia kutatua masuala yanayohusiana na matatizo ya mabadiliko ya tabianchi.

Amesema, serikali ya hivi sasa ya Marekani inafuatilia sana siasa za kuzisambaratisha asasi za serikali kama vile taasisi ya kuhifadhi mazingira na taasisi ya nishati kwa ajili ya kutaka kujiongezea nguvu. Amehoji kwa kusema: "Hivi imewahi kutokea katika historia ya mwanadamu, taasisi kama serikali ya Washington iliyosimama kwa ajili ya kuziangamiza asasi za uhai wa mwanadamu katika uso wa dunia?"

Itakumbukwa kuwa, mwaka jana mwanafalsafa na mtaalamu huyo mkubwa wa lugha nchini Marekani alinukuliwa akitahadharisha sana kuhusu hatua ya chama cha Republican cha Rais Donald Trump ya kutwaa serikali, vyombo vya mahakama na serikali kuu, chama ambacho kwa mtazamo wa Chomsky, ni taasisi hatari sana katika historia ya mwanadamu.

Madhara yanayotokana na tabianchi

Aidha msomi huyo alitabiri kwamba, uongozi wa Trump utakuwa ni pigo kubwa kwa usalama wa dunia hususan katika sekta ya mazingira kwa kuwa rais huyo hana imani yoyote kuhusiana na suala hilo muhimu. Kufuatia misimamo ya ajabu ya serikali ya Rais Donald Trump, Noam Chomsky amesema kuwa, serikali hiyo ambayo haifanyi juhudi yoyote ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, inaelekea kutengwa kimataifa. Itakumbukwa kuwa, mwezi Machi mwaka huu Trump alitoa amri ya kuzuia kutekelezwa siasa za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa zilizoanzishwa na Barack Obama, rais wa zamani wa nchi hiyo.