Jun 04, 2017 04:07 UTC
  • Watu tisa wauawa katika shambulio la kigaidi la London

Watu wasiopungua saba wameuawa na wengine kadhaa kujruhiwa kufuatia shambulio la kigaidi lililotokea katika mji mkuu wa Uingereza London.

Polisi ya London imetangaza kuwa, shambulio hilo lililotokea usiku wa kuamkia leo limepelekea watu tisa kuuawa na wengine 20 kujeruhiwa. Taarifa ya polisi ya London imeeleza kuwa, shambulio hilo ni la kigaidi.

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amesema kuwa, shambulio hilo linatisha na kwamba, baraza lake la mawaziri litakutana leo katika kikao cha dharura kujadili matukio ya kigaidi.

Taarifa ya awali ya polisi ya London inasema kuwa, watu hao wamefariki dunia katika tukio lililohusisha watu kugongwa na gari na wengine kuchomwa visu katika eneo la Daraja la London.

Mmoja wa maafisa usalama akiwa katika eneo la tukio

Maafisa wenye silaha walitumwa eneo hilo baada ya watu walioshuhudia kusema gari la rangi jeupe lilivurumishwa kutoka kwenye barabara na kuwagonga watu waliokuwa wakipita.

Maafisa walitumwa pia katika Soko la Borough, ambapo inadaiwa watu walishambuliwa na kudungwa visu. Ghasia zilianza baada ya gari moja kuingia ndani ya umati wa watembeaji kwa miguu katika daraja kuu jijini London.

Shuhuda mmoja ameziambia duru za habari kwamba, aliwaona watu watatu wakiwa na visu, wakikimbia kutoka katika daraja hilo, kuelekea eneo moja kuliko na soko la Borough. Anasema kuwa watu hao watatu walianza kuwadunga visu watu kiholela barabarani.

Tukio hilo linatokea majuma kadhaa tu baada ya watu 22 kuuliwa pale mhanga mmoja wa kujitolea kufa, alipojilipua ndani ya uwanja mmoja wa burudani huko mjini Manchester.

Tags