Marekani: Tunaweza kushinda vita na Pyongyang, lakini vitakuwa msiba mkubwa
Waziri wa Ulinzi wa Marekani James Mattis amesema kuwa, Washington na washirika wake wanaweza kushinda vita dhidi ya Korea Kaskazini, lakini vita hivyo vitasababisha msiba mkubwa kwa raia wa eneo zima la Korea.
Mattis aliyasema hayo katika ripoti aliyoitoa mbele ya bunge la Kongresi nchini Marekani ambapo sambamba na kubainisha kuwa vita na Korea Kaskazini vinaweza kusababisha maafa makubwa hususan kwa raia wa Japan na Korea Kusini alisema, Washington inatumia uwezo wake wote kuhakikisha vita vya namna hiyo havitokei na badala yake kutatuliwa mzozo uliopo kwa njia ya udiplomasia.
Aidha Waziri wa Ulinzi wa Marekani ameonyesha wasi wasi wake juu ya hatua ya Pyongyang kuweka idadi kubwa ya vifaru na makombora ambayo yanafika mji wa Seoul, mji mkuu wa Korea Kusini na kuongeza kuwa, kabla ya Marekani kuzisambaratisha silaha hizo, kuna uwezekano kwamba zitakuwa zimesababisha hasara kubwa kwa Korea Kusini. Hii ni katika hali ambayo Korea Kaskazini imesisitiza kuwa, itaendelea kujiimarisha kwa miradi yake ya nyuklia na makombora kutokana na siasa za uhasama za Marekani na baadhi ya washirika wake katika eneo. Kwa upande wake Marekani inadai kuwa Pyongyang ni hatari kubwa ambayo inatakiwa kuondolewa haraka kwa ajili ya usalama na amani.
Kabla ya hapo madola ya Magharibi yalitangaza wasi wasi wao kuwa, makombora mapya ya nchi hiyo yanaweza kubeba vichwa vya nyuklia. Inafaa kuashiria kuwa, hadi sasa hali ya eneo la Peninsula ya Korea imezidi kuwa mbaya kutokana na siasa za uhasama za Marekani.