Hotuba ya kifidhuli ya Trump UN yakosolewa vikali duniani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i34607-hotuba_ya_kifidhuli_ya_trump_un_yakosolewa_vikali_duniani
Matamshi ya kifedhuli aliyotoa Rais Donald Trump wa Marekani katika hotuba yake ya kwanza katika mkutano mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) yamekosolewa vikali na viongozi na shakhsia mbalimbali wa kisiasa duniani.
(last modified 2026-04-26T10:08:53+00:00 )
Sep 20, 2017 03:35 UTC
  • Hotuba ya kifidhuli ya Trump UN yakosolewa vikali duniani

Matamshi ya kifedhuli aliyotoa Rais Donald Trump wa Marekani katika hotuba yake ya kwanza katika mkutano mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) yamekosolewa vikali na viongozi na shakhsia mbalimbali wa kisiasa duniani.

Katika hotuba aliyotoa mbele ya viongozi na wawakilishi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa hapo jana, Rais wa Marekani alitumia lugha isiyo ya kawaida wala isiyo ya kidiplomasia kwa kuonyesha msimamo mkali dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Korea Kaskazini, Syria, Venezuela, Cuba na nchi nyengine kadhaa duniani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Muhammad Javad Zarif amesema, hotuba ya kijinga na ya chuki aliyotoa Trump inahusiana na Enzi za Kati (Middle Ages), si karne ya 21 wala haina thamani ya kujibiwa.

Rais Nicolás Maduro wa Venezuela amemtaja Donald Trump kuwa ni "Hitler Mpya" katika siasa za kimataifa.

Kuhusiana na lugha aliyotumia Trump dhidi ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yaliyofikiwa kati ya Iran na nchi zinazounda kundi la 5+1 ikiwemo Marekani yenyewe, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema katika hotuba aliyotoa kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba kuyaua makubaliano hayo ya nyuklia litakuwa ni kosa kubwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif (kulia) na Trump

Aliyekuwa Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden Carl Bildt, yeye mbali na kutangaza uungaji mkono wa nchi yake kwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ambayo Trump ameyakosoa vikali, amesema hotuba ya Rais huyo wa Marekani haikuwa sahihi.

Ben Rhodes, mshauri wa rais wa zamani wa Marekani Barack Obama amekosoa matamshi ya Trump na kuandika kwenye ukurasa wake wa Twitter: "Trump amewafanya waitifaki wetu maajinabi kwa Marekani".

Naye John Kirby, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani katika serikali iliyopita ya nchi hiyo amesema hotuba ya Rais wa Marekani imeifedhehesha nchi hiyo na kubainisha kuwa badala ya Trump kuzungumzia ushirikiano na kuheshimiana baina ya pande mbili anazungumzia ugomvi na mapigano.

Inafaa kuashiria kuwa Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel yeye ameisifu na kuipongeza hotuba iliyotolewa na Rais wa Marekani katika mkutano mkuu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo jana.../