Malumbano ya Rais Trump na viongozi wa chama cha Repulican
https://parstoday.ir/sw/news/world-i35457-malumbano_ya_rais_trump_na_viongozi_wa_chama_cha_repulican
Rais Donald Trump wa Marekani amemshambulia na kumkosoa kwa maneno makali mmoja wa viongozi wenzake wa chama cha Republican katika Kongresi ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 09, 2017 23:39 UTC
  • Malumbano ya Rais Trump  na viongozi wa chama cha Repulican

Rais Donald Trump wa Marekani amemshambulia na kumkosoa kwa maneno makali mmoja wa viongozi wenzake wa chama cha Republican katika Kongresi ya nchi hiyo.

Rais Trump amemshambulia kwa maneno Bob Corker, Mkuu wa Kamati ya Mahusiano ya Kigeni katika Baraza la Seneti katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwa kuandika:  Bob Corker alinipigia simu na kunitaka nimuunge mkono katika uchaguzi wa Seneti. Nikamwambia hapana na hivyo akalazimika kujitoa. Alikuwa akitaka awe Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani, lakini nikamkatalia. Kwa kiwango kikubwa, yeye ni sababu ya kufikiwa makubaliano ya kutisha na Iran.

Malumbano na masutano hayo yaliendelea baada ya Bob Corker naye kujibu mapigo kwa kuandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: Ni izara na fedheha kuona ikulu ya Marekani White imegeuka na kuwa kituo cha kulea watu wazima; na bila shaka mmoja wa wahusika wa kituo hicho leo asubuhi hajaripoti kazini.

Seneta Bob Corkker, Mkuu wa Kamati ya Mahusiano ya Kigeni katika Baraza la Seneti

Hata hivyo hii si mara ya kwanza kwa Rais huyo wa Marekani kuwakosoa katika Kongresi ya nchi hiyo wanachama wenzake wa chama cha Republican. Kuanzia Mitch McConnell, kiongozi wa waliowengi katika Baraza la Seneti hadi kwa John McCain Mkuu wa Kamati ya vikosi vya ulinzi ya Seneta na ambaye aligombea urais kwa tiketi ya chama hicho mwaka 2008. Kwa hakika kuna idadi kubwa ya viongozi na wanachama wa Chama cha Repblican ambao wamekabiliwa na wimbi kubwa la hujuma na mashambulio makali ya maneno ya Rais Trump katika kipindi hiki cha miezi 9 cha kuwa kwake madarakani.

Pamoja na hayo, lugha aliyotumia Trump kumkosoa Bob Corker na jibu la seneta huyo kwa Trump ikilinganishwa na huko nyuma, ni jambo ambalo kwa kweli halijawahi kushuhudiwa. Siku chache zilizopita, Bob Corker alitangaza kuwa, hana mpango wa kushiriki katika uchaguzi mdogo hapo mwakani. Tangazo hilo lilikuwa sawa na kumuachia wazi uwanja Donald Trump ili kwa mara nyingine awashambulie viongozi wa Republican na amtangaze Bob Corker kwamba, ndiye aliyehusika kupasishwa "sheria ya kuangalia upya makubaliano ya nyuklia na Iran inayojulikana kama ''Corker–Cardin".   

Rais Donald Trump wa Marekani

Siku chache zijazo, Trump atalazimika kutangaza tena msimamo wake kwa mara ya tatu na kwa mujibu wa sheria hiyo kuhusiana na makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana Rais Trump ameanzisha hujuma na vita vya maneno dhidi ya Corker akifanya juhudi za kujivua kikamilifu jukumu la kutekeleza sheria ya "Corker–Cardin".

Pamoja na hayo malumbano na urushianaji maneno makali baina ya Trump na viongozi wa Republican yamezusha anga ya mvurugiko ndani ya chama hicho na vile vile katika medani ya siasa za Marekani. Licha ya kuwa, nguzo mbili kuu yaani serikali na Bunge zinadhibitiwa na chama kimoja nchini humo, lakini miamala ya kimirengo ya serikali na Bunge ya chama hicho baina yao inashabiana kabisa na ushindani au malumbano ya kisiasa ya vyama viwili hasimu.

Hii ni katika hali ambayo, baadhi ya ahadi muhimu za Warepublican walizozitoa mwaka jana katika kampeni za uchaguzi zimekwama utekelezaji wake kutokana na vita hivi vilivyopo ndani ya chama.

Mpango wa afya wa "Obamacare".

Katika kipindi cha miezi 9 tangu Rais Trump aingine katika ikulu ya Marekani White House,  Baraza la Seneti  linalodhibitiwa na Warepublican, hadi sasa halijapigia kura hata pendekezo moja miongoni mwa mapendekezo ya ikulu ya White House.

Hii ni katika hali ambayo, wananchi wa Marekani hususan wapiga kura waliokichagua chama cha Republican  wanasubiri hatima ya mipango mbadala kama mpango wa afya wa Obamacare au mipango ya kodi, uhajiri na usalama ijulikane haraka sana. Kuendelea hali hii kunaweza kuwachanganya raia wa nchi hiyo na hivyo kuzifanya kura za Warepulican zigawanyike katika uchaguzi mdogo wa 2018 au uchaguzi ujao wa Rais hapo mwaka 2020.