Marekani kujiondoa UNESCO Disemba mwaka huu
Marekani imetangaza kuwa itajiondoa kwenye Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kuanzia Disemba 31 mwaka huu.
Taarifa ya Idara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo imesema Washingon imefikia uamuzi huo, kutokana na kile inachodai kuwa ni misimamo iliyo dhidi ya Israel ya shirika hilo.
Taarifa hiyo iliyotolewa leo Alkhamisi imeongeza kuwa, Washington italiomba shirika hilo la UN liiorodheshe Marekani kama mwanachama mtazamaji tu.
Mwaka uliopita, uamuzi wa UNESCO wa kusisitiza kuwa Mayahudi hawana uhusiano wowote ule na Masjidul Aqsa, ambacho ni Kibla cha kwanza cha Waislamu, wala mji wa Quds, uliwakasirisha sana viongozi wa utawala wa Kizayuni na Marekani.
Shirika hilo la UN wakati huo lilipasisha muswada uliosisitiza kuwa, hakuna uhusiano wowote wa kihistoria, kidini wala wa kiutamaduni uliopo baina ya Mayahudi na maeneo matakatifu katika mji wa Quds ukiwemo Msikiti wa al-Aqsa.
UNESCO mbali na kulaani vitendo vya Wazayuni vya kupotosha asili ya kihistoria ya Quds, pia ulisisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unapaswa kuacha kujitanua na kufanya vitendo vya ukatili katika maeneo ya watu wengine.