RSF: Wanahabari 65 wameuawa wakiwa kazini mwaka huu 2017
Shirika la Maripota Wasio na Mipaka (RSF) limesema jumla ya waandishi wa habari na wafanyakazi wengine katika sekta ya upashanaji habari 65 wameuawa mwaka huu 2017 katika sehemu mbali mbali duniani.
Katika ripoti yake ya kila mwaka, shirika hilo lenye makao yake nchini Ufaransa limeitaja Syria kama nchi hatari zaidi kwa usalama wa waandishi wa habari, ambapo wanahabari 12 ni miongoni mwa makumi waliouawa kote duniani mwaka huu.
Kwa mujibu wa shirika hilo, Mexico ndiyo nchi ya pili kwa kushuhudia mauaji ya kiholela ya waandishi wa habari, ambapo 11 wameuawa mwaka huu pekee, hususan waliokuwa wakifuatilia kashfa za ufisadi wa kisiasa na jinai za kuratibiwa.
Shirika hilo limetangaza kuwa, waandishi habari katika baadhi ya nchi za Afrika hawana uhuru wa kujieleza na wanafanya kazi katika mazingira ya mashinikizo na ukandamizaji.
Ripoti ya Shirika la Maripota Wasio na Mpaka imeashiria hali ya waandishi wa habari katika nchi za Afrika kama Libya, Mali na Guinea Conakry na kusema waandishi hao hawana usalama wala amani.
Kwa mujibu wa Federesheni ya Kimataifa ya Waandishi Habari (IFJ), waandishi habari 93 waliuawa kwa makusudi au katika machafuko yaliyotokea kwenye maeneo mbalimbali ya dunia mwaka jana 2016.