Kongresi yataka kuchunguzwa uhusiano wa mkwe wa Trump na Bin Salman
(last modified Fri, 30 Mar 2018 08:13:41 GMT )
Mar 30, 2018 08:13 UTC
  • Kongresi yataka kuchunguzwa uhusiano wa mkwe wa Trump na Bin Salman

Wajumbe kadhaa wa Kongresi ya Marekani wameiandikia barua Idara Polisi ya Federali ya nchi hiyo (FBI) wakitaka kufanyike uchunguzi juu ya uhusianio uliopo baina ya mkwe wa Rais Donald Trump wa nchi hiyo na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman.

Wabunge Ted Lieu, Gerald Connolly, Donald Beyer,  Pramila Jayapal, Peter Welch, Ruben Gallego wa chama cha Democratic wameiandikia barua polisi ya FBI wakitaka ianzishe uchunguzi na kubaini mahusiano yaliyopo baina ya Jared Kushner na Bin Salman.

Wabunge wa chama cha Democratic wana wasiwasi kwamba, mkwe huyo wa Donald Trump amevujisha baadhi ya ripoti za siri za White House kutokana na uhusiano wake wa karibu na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia. 

Mtandao wa habari wa The Intercept umeripoti kuwa, katika mazungumzo yake ya mwaka jana na Bin Salman, Jared Kushner alifichua habari za siri kuhusu wanasiasa mashuhuri wanaompinga Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia. 

Jared Kushner

Maafisa wa Ikulu ya Rais wa Marekani, White House wana wasiwasi kwamba, mtandao tata wa mahusiano ya kibiashara ya Kushner yanaweza kutumiwa na nchi za kigeni kama fimbo ya mashinikizo dhidi ya serikali ya Washington. Ripoti zinasema kuwa, katika siku za hivi karibuni maafisa wa Imarati, China, Mexico na utawala wa Kizayuni wa Israel walikutana kwa siri na kufanya mazungumzo na mkwe huyo wa Donald Trump kwa shabaha ya kutumia ushawishi wake ndani ya White House.