Apr 30, 2018 04:06 UTC
  • Meya wa London: Trump inabidi aombe radhi rasmi

Meya wa jiji la London Sadiq Khan amemtaka Rais Donald Trump wa Marekani atoe tamko rasmi la kuomba radhi.

Khan, ambaye ni mmoja wa wapinzani wakubwa wa Trump ametoa wito huo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya ITV na kubainisha kuwa, wakati wa safari yake nchini Uingereza, itabidi Trump aombe radhi rasmi kwa kitendo chake cha kusambaza tena kupitia ukurasa wake wa twitter mikanda ya vidio zinazoeneza chuki dhidi ya Uislamu iliyotolewa na kundi lenye misimamo ya kufurutu mpaka liitwalo "Uingereza Kwanza".

Meya wa jiji la London ameongeza kuwa, lengo la kundi la harakati za kundi la Uingereza Kwanza (Britain First) ni kupanda mbegu za unafiki na mpasuko katika jamii.

Sadiq Khan, Meya wa jiji la London

Sambamba na kuashiria kuwa kwa baraka za urais wa Trump anga ya chuki imetanda kwenye jamii ya Marekani, Sadiq Khan amebainisha kuwa mwasisi wa uenezaji chuki ndani ya Uingereza sasa ametoa mwaliko kwa mwasisi wa uenezaji chuki ndani ya Marekani.

Mnamo mwezi Novemba mwaka jana, Trump alisambaza tena kupitia ukurasa wake wa kijamii wa twitter mikanda ya vidio iliyowahi kusambazwa hapo kabla na kundi la Uingereza lenye misimamo ya chuki dhidi ya Uislamu la Uingereza Kwanza.

Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, rais huyo wa Marekani ameakhirisha mara tatu safari aliyokuwa amepanga kufanya ya kuitembelea Uingereza kutokana na hasira za fikra za waliowengi nchini humo dhidi ya sera zake, zikiwemo za ubaguzi.

Trump sasa anatazamiwa kufanya safari nchini Uingereza tarehe 13 Julai mwaka huu.../

Tags