May 18, 2018 08:12 UTC
  • Rais wa Uturuki: Marekani imekosea kujiondoa katika JCPOA

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesema kuwa kitendo cha Marekani kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya Iran JCPOA ni makosa, na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni chanzo cha kushadidi mgogoro na ukosefu wa amani katika eneo.

Akiashiria maelfu ya vichwa vya silaha za nyuklia vilivyorundikwa katika maghala ya kuhifadhia silaha za atomiki ya nchi zinazomiliki silaha hizo ikiwemo Marekani, Rais Erdoğan amesema kuwa katika mazingira kama hayo kitendo cha kuibua tuhuma dhidi ya miradi ya amani ya nyuklia ya Iran, hakina lengo jingine ghairi ya kuizidishia mashinikizo Tehran. 

Baadhi ya mabomu ya nyuklia ya Marekani yakiwa yamehifadhiwa katika maghala

Erdoğan ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya BBC ambapo pamoja na mambo mengine amekosoa hatua ya upande mmoja ya Washington ya kujiondoa katika mapatano ya kimataifa ya JCPOA na kuongeza kwamba, uvunjaji ahadi wa Marekani ulioshuhudiwa katika kadhia hiyo, utalisababishia mivutano zaidi eneo. Amezidi kusisitiza kwamba, kamwe Marekani haikuwahi kulitilia umuhimu wowote eno la Mashariki ya Kati na katika uwanja huo Washington imekuwa ikipuuza masuala muhimu na kwamba hatua ya Trump ya kuiondoa nchi yake katika mapatano hayo ya nyuklia ya Iran itasababisha kuibuka ushindani wa silaha katika eneo tajwa.

Rais Donald Trump wa Marekani na uvunjaji wake wa mikataba ya kimataifa

Makubaliano ya nyuklia ya Iran kwa kifupi JCPOA yalifikiwa mjini Vienna, Austria yapata miaka mitatu iliyopita kwa kuzihusisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi za kundi la 5+1 yaani (China, Ufaransa, Russia, Uingereza, Marekani na Ujerumani.) Hata hivyo tangu alipoingia madarakani Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa akiyakiuka na hatimaye hivi karibuni alitangaza rasmi kujitoa moja kwa moja nchi yake katika makubaliano hayo. 

Tags