Jun 11, 2018 07:16 UTC
  • Waislamu Austria walaani azma ya serikali ya kutaka kufunga misikiti nchini

Waislamu nchini Austria wamekosoa vikali mpango wa serikali wa kufunga misikiti saba na kuwatimua makumi ya Maimamu na familia zao kutokana na kile inachodai ni mkakati wa kuzuia 'Uislamu wa kisiasa' katika nchi hiyo ya Ulaya.

Shirikisho Kuu la Waislamu nchini humo (IGGiOe) limesema mpango huo wa serikali unanuia kudhoofisha umma wa Kiislamu ambao ni katika jamii za walio wachache katika nchi hiyo.

Rais wa shirikisho hilo Ibrahim Olgun ameikosoa vikali serikali kwa kuchukua hatua hiyo ya upande mmoja bila kuishauri, tena katika Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Amesema jumuiya hiyo ya Waislamu wa Austria itafanya tathmini ya kina juu ya misikiti saba ambayo serikali inapania kuifunga, na pia kukutana na Maimamu 60 ambao wanafadhiliwa na Uturuki na ambao serikali inapanga kuwatimua, kabla ya kuitisha mkutano na Waziri wa Utamaduni wa nchi hiyo.

Maandamano yaliyofanyika huko nyuma baada ya Austria kupiga maruku hijabu

Wakati huo huo, Rais Reccep Tayyip Erdogan wa Uturuki sanjari na kulaani mpango huo wa serikali ya Vienna, amesema iwapo utatekelezwa yumkini ukaitumbukiza nchi hiyo ya Ulaya katika vita vya kidini anavyovitaja kama vita kati ya Msalaba na Hilali. 

Ijumaa iliyopita, Kansela wa Austira Sebastian Kurz alisema serikali yake itafunga misikiti saba inayofadhiliwa na Uturuki mbali na kubatilisha kibali cha Jumuiya ya Kidini ya Waarabu ambayo inasimamia misikiti hiyo na Maimamu wake.

Tags