UN yatahadharisha kuhusu uchafuzi wa hali ya hewa duniani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i46132-un_yatahadharisha_kuhusu_uchafuzi_wa_hali_ya_hewa_duniani
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusu ongezeko la uchafuzi wa hali ya hewa na hatari zake kwa viumbe kote duniani.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jun 21, 2018 03:45 UTC
  • UN yatahadharisha kuhusu uchafuzi wa hali ya hewa duniani

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusu ongezeko la uchafuzi wa hali ya hewa na hatari zake kwa viumbe kote duniani.

Ripoti ya Malengo ya Ustawi Endelevu 2018 iliyotolewa jana katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York imesema kuwa, mwaka 2016 asilimia 91 ya jamii ya watu wanaoishi mijini kote duniani walitumia hewa ambayo haikuwa na viwango vilivyoainishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Ripoti hiyo imesema kuwa, zaidi ya nusu ya jamii hiyo ya watu wa dunia wanasumbuliwa na hali ya hewa chafu mara mbili zaidi ya kiwango kilichoainishwa. 

Uchafuzi wa hali ya hewa mijini

Sehemu nyingine ya ripoti hiyo imesema kuwa, katika kipindi cha baina ya mwaka 2000 na 2014 jamii ya watu wa mjini waliokuwa wakiishi katika maeneo yasiyofaa na yenye msongamano mkubwa wa watu duniani ilifikia milioni 883.

Marekani imetajwa kuwa ya kwanza kati ya nchi zilizoendelea kiviwanda kwa kuchafua mazingira na hali ya hewa.

Pamoja na hayo Rais Donald Trump wa Marekani ameiondoa nchi hiyo katika Mkataba wa Hali ya Hewa wa Paris licha ya malalamiko makubwa ya jamii ya kimataifa.