Zarif: Wamarekani wamechoshwa na udhalimu wa viongozi wao
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema wananchi wa Marekani wamechoshwa na ufisadi, udhalimu, ukosefu wa uadilifu na kutostahiki watawala wao.
Huku akibaini kuwa walimwengu wamesikia kilio cha Wamarekani, Mohammad Javad Zarif amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani vikali sera za Marekani za kuwakandamiza wananchi, kuwafunga jela waandamanaji, kuwatenganisha wahajiri na familia zao na kuwaweka kizuizini watoto wadogo.
Mike Pompeo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Jumatano akiwa katika Bunge la Senate nchini humo alisema anafanya mazungumzo na wenzake wa Ulaya kuhusu kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Aidha alidai kuwa Marekani ina uwezo wa kupunguza ushawishi wa Iran nchini Iraq.
Katika kujibu madai hayo na tuhuma dhidi ya Iran, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa, Marekani inaharibu fedha za walipa kodi Wamarekani na kuongeza kuwa: "Chokochoko za Marekani Iraq na Afghanistan na uungaji mkono wake kwa utawala wa Israel unaoua watoto na tawala zingine zinazounga mkono magaidi katika eneo na usambazaji wa zana zake za nyuklia ni mambo ambayo yanagharimu kiasi kikubwa cha fedha na hivyo kuwasababishia Wamarekani masaibu na matatizo mengi ya kimasiha.
Zarif amesema si jambo la kushangaza kuona maandamano ya wananchi yakienea kote Marekani kwa sababu, "Wamarekani wamechoshwa na watawala wao na wanataka utajiri wa Marekani utumiwe kukidhi mahitaji halali ya wananchi. Hivi sasa Wamarekani milioni 40, katika nchi hiyo tajiri zaidi duniani, wanaishi chini ya mstari wa umasikini.."