Jul 05, 2018 03:39 UTC
  • Waislamu Warohingya 11,432 wamekimbia ukandamizaji Myanmar mwaka 2018

Waislamu Warohingya wasiopungua 11,432 wamekimbia ukandamizaji wanaotendewa nchini Myanmar na kupata hifadhi katika nchi jirani ya Bangladesh.

Hayo yamedokezwa na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad al-Hussein. Akihutubu Jumatano katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa alisema Waislamu wanaendelea kukimbia ukandamizaji nchini Myanmar katika jimbo la Rakhine huku wengi wakitoa ushuhuda wa ukandamizaji, dhulma na mauaji yanayotekelezwa dhidi yao.

Disemba mwaka jana Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alisema kuwa uhalifu unaofanywa na Mabudha nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ni mauaji ya kimbari.

Ra'ad Al Hussein amesema kuwa, Waislamu wa Rohingya wanalengwa na kuuawa kwa sababu ya utambulisho wao na kwamba wananyimwa hata haki ya kuwa na majina ya Kiislamu. 

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad al-Hussein

Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi nchi hiyo tangu tarehe 25 Agosti mwaka jana hadi sasa. 

Mauaji hayo ya umati dhidi ya Waislamu nchini Myanmar yamepelekea zaidi ya Waislamu laki saba kukimbilia hifadhi katika nchi jirani ya Bangladesh.

Jinai za jeshi la Myanmar na Mabudha wa nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya zinaendelea katika hali ambayo, serikali ya nchi hiyo iliahidi kuandaa mazingira ya kurejea makwao wakimbizi wa Kirohingya.

 

Tags