HRW: Wasimamizi wa kimataifa wakague jela za Saudia, wanawake wanabakwa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i50032-hrw_wasimamizi_wa_kimataifa_wakague_jela_za_saudia_wanawake_wanabakwa
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limetoa wito wa kupelekwa wakaguzi huru wa kimataifa nchini Saudi Arabia kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa wanaharakati wanaoshikiliwa katika jela za nchi hiyo hususan wanawake ambao baadhi ya ripoti zinasema wanateswa na hata kubakwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 08, 2018 06:12 UTC
  • HRW: Wasimamizi wa kimataifa wakague jela za Saudia, wanawake wanabakwa

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limetoa wito wa kupelekwa wakaguzi huru wa kimataifa nchini Saudi Arabia kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa wanaharakati wanaoshikiliwa katika jela za nchi hiyo hususan wanawake ambao baadhi ya ripoti zinasema wanateswa na hata kubakwa.

Ripoti iliyotolewa na Human Rights Watch imesema kuwa, wanaharakati wa masuala ya kijamii wanateswa na kushikiliwa jela bila ya kuambiwa makosa yao na kwamba kuna udharura wa kutumwa wakaguzi huru wa kimataifa kujua hali ya usalama wao na kuhakikisha wahusika wa uhalifu huo wanachukuliwa hatua.

Ripoti ya Human Rights Watch pia imeashiria urongo uliosemwa na maafisa wa Saudi Arabia baada ya mauaji ya mwandishi habari na mkosoaji wa utawala wa nchi hiyo Jamal Khashoggi na kusisitiza kwamba, kuna udharura wa kufanyika uchunguzi kuhusu hali ya mahabusu na watetezi wa haki za binadamu wanaoshikiliwa katika jela za Saudia na kuwachukulia hatua maafisa wanaofanya uhalifu wa kuwatesa na kuwanyanyasa wanaharakati hao.

Wito wa Human Righs Watch umetolewa baada ya kuvuja ripoti kwamba, Saud al Qahtani aliyekuwa mshauri wa Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa nchi hiyo mbaye pia aliongoza timu iliyohusika na mauaji ya Jamal Khashoggi mjini Istanbul alisimamia mateso na unyanyasaji uliofanywa dhidi ya mwanaharakati wa kike wa nchi hiyo na akatishia kumbaka na kumuua. Ripoti hiyo pia imesema wasaidizi wa al Qahtani waliwatesa mahabusu wengine wa kike na kuwanajisi.

Al Qahtani na Bin Salman

Mwishoni mwa wiki iliyopita shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty international lilieleza wasiwasi wake kuhusu sera za kuwakandamiza wanaharakati wa kisiasa, waandishi habari na wasomi wa vyuo vikuu nchini Suaudi Arabia na vilevile kutiwa nguvuni, kuteswa wanaharakati wa kike.