Baraza Kuu la UN lapasisha azimio dhidi ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i50311-baraza_kuu_la_un_lapasisha_azimio_dhidi_ya_marekani
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepasisha azimio linaloitaka Marekani kukomesha hatua zilizo kinyume na sheria dhidi ya wawakilishi na maeneo ya kidiplomasia ya Russia nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 21, 2018 01:08 UTC
  • Baraza Kuu la UN lapasisha azimio dhidi ya Marekani

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepasisha azimio linaloitaka Marekani kukomesha hatua zilizo kinyume na sheria dhidi ya wawakilishi na maeneo ya kidiplomasia ya Russia nchini humo.

Ofisi ya mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa, azimio lililopasishwa na Baraza Kuu la umoja huo ambalo limependekezwa na Kamati yake ya Sita limekosoa waziwazi hatua zinazochukuliwa na Marekani dhidi ya wanadiplomasia na maeneo ya kidiplomasia ya Russia. Azimio hilo limeitaka Marekani kukomesha mara moja hatua zisizo za kisheria dhidi ya ofisi ya mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa na maeneo ya kidiplomaia ya nchi hiyo mjini New York. Azimio hilo limezungumzia masuala kama kutwaliwa mali za ofisi ya mwakilishi wa Russia mjini New York, kubanwa uhuru wa kutembea wa baadhi ya wafanyakazi wa ofisi hiyo na matatizo ya kupewa visa wanadiplomasia wa Russia katika Umoja wa Mataifa. 

Itakumbukwa kwamba, mwezi Machi mwaka huu wa 2018 Marekani iliwafukuza wanadiplomasia 48 na wafanyakazi 12 wa ofisi ya mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa mjini New York na ikafunga ofisi ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo katika jimbo la Seattle. 

Sergei Skripal

Hatua hiyo ilichukuliwa na Marekani sambamba na Uingereza na nchi nyingine kadhaa za Ulaya kwa madai kuwa, Russia ilihusika la jaribio la kumuua kwa sumu jasusi wa zamani wa nchi hiyo, Sergei Skripal nchini Uingereza. Russia imekanusha madai hayo.