Apr 12, 2019 04:29 UTC
  • Maandamano yashuhudiwa London baada ya kukamatwa mwasisi wa Wikileaks

Maandamano yameshuhudiwa nje ya ubalozi wa Ecuador mjini London baada ya polisi ya Uingereza kumtia mbaroni mwasisi wa mtandao unaofichua fedheha nyingi za nchi na viongozi mbalimbali duniani wa WikiLeaks, Julian Assange, ambaye amekuwa akiishi ubalozini hapo tokea mwaka 2012.

Baadhi ya waandamanaji walikuwa wamebeba mabango yenye jumbe zinazosema, "Muachilieni huru Julian Assange", "Assange, mteule wa Tuzo ya Amani ya Nobel" na "Sisi ni Assange". Mmoja wa waandamanaji na mfuasi wa mwasisi huyo wa mtandao wa kufichua uozo serikali amesema, "Leo ni siku ya fedheha katika mfumo wa sheria wa Uingereza." Julian Assange alikamatwa jana na maaafisa wa polisi wa mjini London, muda mfupi baada ya Rais wa Ecuador kubatilisha kibali cha kumpa hifadhi mwandishi huyo wa habari ambaye ameishi katika ubalozi wa Ecuador mjini London kwa miaka saba.  Oktoba mwaka jana, mtandao wa WikiLeaks ulifichua kuwa, magazeti ya Uingereza halikataa kuakisi habari za mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari mkosoaji wa utawala wa Saudi Arabia aliyeuliwa katika ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul, Uturuki, kwa kuwa yamemwagiwa pesa na utawala wa Riyadh.

Julian Assange

Wakili wa Assange, Jen Robinson amesema kuwa, mteja wake amekamatwa pia kutokana na ombi la Marekani ambayo inataka apelekwe nchini humo kwa ajili ya kufunguliwa mashitaka ya kuvujisha nyaraka za serikali. Mtandao huo wa Wikileaks uliosisiwa na Julian Assange umekuwa ukifichua uozo wa serikali ya Washington, ikiwemo video aliyoivujisha iliyoonesha mauaji ya kiholela yaliyofanywa na jeshi la Marekani iitwayo "Collateral Murder". Mwishoni mwa mwaka jana, mtandao huo ulifichua pia kuwa, balozi za Marekani na vituo vingine vyake vya kidiplomasia kote duniani vimenunua kiwango kikubwa cha vifaa na suhula za kijasusi; katika hali ambayo baadhi ya nchi zimekuwa zikieleza hofu yao kwamba balozi hizo za Marekani badala ya kujihusisha na masuala ya udiplomasia pamoja na uhusiano mwema, zinahusika zaidi na masuala ya ujasusi, mapinduzi ya serikali halali na njama zinginezo haribifu kote duniani.

Tags