Jun 07, 2019 03:05 UTC
  • Wasiwasi wa wakimbizi Warohingya nchini Bangladesh kuhusu watoto wao

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR linafanya kila liwezalo kuhakikisha watoto wakimbizi Warohingya huko Bangladesh wanapata elimu wakati huu ambapo wazazi wao wana hofu kubwa juu ya mustakabali wa elimu ya watoto hao.

UNHCR inasema kuwa zaidi ya nusu ya wakimbizi wote 620,000 Warohingya kutoka Myanmar ambao wanaishi kwenye makazi ya Cox’s Bazar, kusini-mashariki mwa Bangladesh ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 18.

UNHCR inasema asilimia 39 ya watoto Warohingya wenye umri wa kati ya miaka 3 hadi 14 na asilimia 91 ya vijana bado hawana fursa ya kujifunza kwenye makazi hayo yaliyojaa pomoni.

Hata hivyo UNHCR tayari imechukua hatua kwa kufungua kituo cha kujifunza kwa watoto kwenye makazi ya wakimbizi ya Kutupalong wakifundishwa hesabu, kiingereza na lugha ya Myanmar.

Watoto Warohingya katika kambi ya wakimbizi

Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi nchi hiyo tangu tarehe 25 Agosti mwaka 2017 hadi sasa. Mauaji hayo ya umati dhidi ya Waislamu nchini Myanmar yamepelekea karibu Waislamu milioni moja wa jamii ya Rohingya kukimbilia hifadhi katika nchi jirani ya Bangladesh.

 

Tags