Warohingya 60,000 wawasili Bangladesh kufuatia kupamba moto mzozo nchini Myanmar
Huku kukiwa na mzozo kati ya serikali ya kijeshi na jeshi la waasi la Arakan nchini Myanmar, Waislamu wa kabila la Rohingya wapatao 60,000 wamewasili Bangladesh katika muda wa miezi miwili iliyopita.
Bangladesh imetoa hifadhi kwa wakimbizi milioni 1.2 wa Kirohingya katika wilaya yake ya kusini-mashariki ya Cox's Bazar. Waislamu wengi wa kabila la Rohingya walikimbilia Bangladesh wakitokea nchini kwao Myanmar mwezi Agosti mwaka 2017 wakikwepa ukandamizaji na mauaji ya jeshi la nchi hiyo.

Wimbi la raia hao la kuingia nchini Bangladesh pia limekuwa likiwezeshwa na ufisadi unaoshuhudiwa katika mpaka wa nchi hiyo na Mynmar ambapo baadhi ya watu huwasaidia wakimbizi ha kuvuka mpaka ili kuingia Bangladesh mkabala wa kupatiwa pesa.
Touhid Hossain Mshauri wa Masuala ya Kigeni wa Bangladesh amesema kuwa msimamo wa serikali ya nchi hiyo ni kutowaruhusu raia wengine wa Kirohingya kuingia Bangladesh. Amesema: "Hata hivyo wakati mwingine hali ya mambo inatufanya tuwapokea wakimbizi hao. Ndio maana tumekubali Waislamu wa Rohingya elfu sitini kuingia Bangladesh. Si kwamba tuliwaruhusu kuingia rasmi, waliingia kupitia njia tofauti”.
Itakumbukwa kuwa jeshi la waasi wa Mynmar la Arakani sasa linadhibiti maeneo mengi katika jimbo la Rakhine karibu na mpaka wa Bangladesh.