China yakosoa kuendelea vikwazo vya Marekani dhidi ya mashirika yake
Msemaji wa Wizara ya Biashara ya China amesisitizia udharura wa kuondolewa vikwazo vya Marekani dhidi ya mashirika ya nchi hiyo.
Sambamba na kupinga kupeda makubwa kwa Marekani katika uga wa kudhibiti uuzaji nje bidhaa, Gao Feng amesema kuwa Washington ni lazima iyaondolee haraka vikwazo mashirika ya China likiwemo la Huawei. Hii ni katika hali ambayo Jumatano iliyopita Rais Donald Trump wa Marekani aliionya Beijing kwamba iwapo mazungumzo yake na Rais Xi Jinping wa China yatafeli, basi atazipandishia ushuru wa forodha bidhaa zote za China zinazoingizwa Marekani. Kufuatia indhari hiyo, Gao Feng, Msemaji wa Wizara ya Biashara wa China amesema kuwa, iwapo mashirika ya kigeni yataendeleza hatua zao za ubaguzi dhidi ya mashirika ya Kichina, Beijing pia itayaweka mashirika hayo katika orodha yake ya mashirika yasiyoaminika.
Hivi karibuni serikali ya Marekani ilizipandishia ushuru wa forodha wa asilimia 10 ambao ni sawa na Dola bilioni 200 bidhaa za China na kuufikisha asimilia 25. Kufuatia hatua hiyo, serikali ya China pia ikazipandishia ushuru wa Dola bilioni 60 bidhaa za Marekani zinazoingizwa nchi hiyo, kutoka asilimia 10 hadi 25. Msuguano wa China na Marekani ulianza tarehe 8 Machi 2018, baada ya Trump kuzipandishia ushuru wa forodha bidhaa za China.