Zarif: Marekani haitafika popote kwa kupenda makuu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i54877-zarif_marekani_haitafika_popote_kwa_kupenda_makuu
Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Marekani haitafika popote kwa kupenda makuu na pia kutokana na tabia yake ya kuendelea kuiwekea mashinikizo Tehran.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 20, 2019 07:35 UTC
  • Zarif: Marekani haitafika popote kwa kupenda makuu

Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Marekani haitafika popote kwa kupenda makuu na pia kutokana na tabia yake ya kuendelea kuiwekea mashinikizo Tehran.

Dakta Zarif alisema hayo mbele ya waandishi wa habari mjini Washington Ijumaa ya jana kabla ya kuelekea Caracas, mji mkuu wa Venezuela na kubainisha kuwa, makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni mapatano yenye mantiki.

Amebainisha kuwa, "Azma ya Trump ya kulitaka taifa hili lisitishe urutubishaji wa madini yake ya urani itagonga mwamba. Washauri wake wanaompotosha kwa maneno hayo wangelipaswa kumpa ushauri huo miaka ya 2000. Wakati huo jitihada za Marekani za kutaka kuweka kiwango cha urutubishaji wa urani hapa nchini kiwe katika kiwango cha sifuri zilizogonga ukuta, licha ya kufanya Iran na Umoja wa Ulaya zishindwe kufikia muafaka katika jambo hilo." 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa,  iwapo nchi za Ulaya zina hamu ya kweli ya kuyanusuru mapatano ya JCPOA, basi hazina budi kuhakikisha kuwa mfumo maalumu wa mabadilishano ya fedha kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Ulaya (INSTEX) umeanza kufanya kazi.

Trump aliiondoa Marekani kwenye JCPOA akidai kuwa ndio makubaliano mabaya zaidi kwa Washington

Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa akitumia mashinikizo makali zaidi na vitisho ili kwa dhana yake ailazimishe Iran ikubali kukaa katika meza ya mazungumzo na Washington.

Hata hivyo Iran imesimama kidete na kwa nguvu zake zote na hivyo kufanikiwa kusambaratisha njama zote za Washington dhidi yake.