Mpangaji wa mashambulizi ya Septemba 11: Nitatoa ushahidi dhidi ya Wasaudi
Mpangaji wa mashambulizi ya Septemba 11 nchini Marekani amesema kuwa yupo tayari kutoa ushahidi dhidi ya viongozi wa Saudia iwapo serikali ya Marekani haitamhukumu adhabu ya kifo.
Televisheni ya al Jazeera imeripoti kuwa, Khalid Sheikh Mohammed ambaye anatajwa kuwa mpangaji wa mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001 huko Marekani amesema kuwa yupo tayari kuzisaidia na kushirikiana na familia za wahanga wa matukio hayo kufuatilia haki zao za kisheria huko Saudia kukiwemo kulipwa fidia iwapo Marekani itatupilia mbali kumhukumu kifo.
Khalid Mohammed Sheikh ni mmoja wa wanachama wa ngazi ya juu wa mtandao wa kigaidi wa al Qaida ambaye alitiwa mbaroni nchini Pakistan mwaka 2003.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, familia za wahanga wa mashambulizi ya Septemba 11 nchini Marekani Ijumaa iliyopita ziliituhumu Saudi Arabia kuwa ndiyo iliyoratibu utekelezaji wa mashambulizi hayo. Katika upande mwingine, Rais Donald Trump wa Marekani jana alisaini sheria ya kuzilipa fidia familia za wahanga wa mashambulizi hayo. Sheria hiyo inaeleza kuwa, serikali ya Marekani itatoa fidia hadi miaka 73 ijayo kwa mtu yoyote aliyedhurika na mashambulizi ya Septemba 11 au familia za wahanga wa mashambulizi hayo.
Watu zaidi ya elfu tatu waliuliwa na elfu sita kujeruhiwa katika mashambulizi ya Septemba 11 nchini Marekani ambapo viongozi wa Saudi Arabia wanatuhumiwa kushirikiana na wapangaji na watekelezaji wa mashambulizi hayo ambapo ndege ya abiria iliyokuwa imetekwa nyara na magaidi hao ilitumika kubomoa na kusababisha mlipuko katika minara pacha ya jengo la biashara la World Trade Center mjini New York.