UN yatahadharisha juu ya kuendelea mashambulizi ya magaidi huko Syria
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa kundi la kigaidi la Jabhatul Nusra lingali linaendelea kuwashambulia wananchi wa Syria.
Mark Lowcock Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Anayeshughulikia Masuala ya Kibinadamu amesema kuwa kuendelea kuuliwa raia wa Syria katika mashambulizi yanayofanywa na makundi ya kigaidi likiwemo kundi la Jabhatul Nusra nchini humo ni jambo lenye kutia wasiwasi. Lowcock aliyasema hayo jana katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichoitishwa kujadili hali ya kibinadamu huko Syria.
Lowcock ameongeza kuwa raia wa Syria wasiopungua 450 wameuawa katika mashambulizi ya ufyatuaji risasi ya kundi la kigaidi la Jabhatul Nusra na makundi mengine ya kigaidi tangu mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu. Amesema kuwa mamia ya raia wengine wamejeruhiwa na zaidi ya laki nne na elfu arubaini wamekuwa wakimbizi. Lowcock ameashiria pia barua ya serikali ya Syria inayoeleza kwamba kuna hospitali 119 katika mkoa wa Idlib kaskazini magharibi mwa nchi hiyo ambazo zinashikiliwa na magaidi; na hazitumiki tena kama hospitali.
Zaidi ya watu milioni 12 huko Syria wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mgogoro wa miaka minane ulioiathiri nchi hiyo.