Facebook yafunga akaunti na kurasa bandia zinazoihusu Riyadh
https://parstoday.ir/sw/news/world-i55149-facebook_yafunga_akaunti_na_kurasa_bandia_zinazoihusu_riyadh
Mtandao wa kijamii wa Facebook umefunga hesabu bandia zaidi ya 350 zenye mfungamano na Saudi Arabia ambazo baadhi zina wafuasi zaidi ya milioni moja na laki nne.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 02, 2019 20:56 UTC
  • Facebook yafunga akaunti na kurasa bandia zinazoihusu Riyadh

Mtandao wa kijamii wa Facebook umefunga hesabu bandia zaidi ya 350 zenye mfungamano na Saudi Arabia ambazo baadhi zina wafuasi zaidi ya milioni moja na laki nne.

Mtandao wa Facebook umetangaza kuwa kurasa na hesabu hizo bandia zenye mfungamano na Saudia kazi yake ni kuifanyia propaganda serikali ya Riyadh lengo likiwa ni kuwalenga wapinzani. Hii ni mara ya kwanza ambapo Saudia imenyooshewa waziwazi lawama na mtandao wa Facebook. 

Katika miaka ya karibuni kulianzishwa kurasa mbalimbali katika mitandao ya kijamii kama Facebook na Twitter kwa lengo la kumpigia propaganda Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia na kuwachafua wapinzani wa utawala wa Aal Saud. Kurasa hizo zilianzishwa kwa amri ya Saud al Qahtani, mshauri wa ngazi ya juu wa Muhammad bin Salman Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia. Qahtani ni mmoja wa watuhumiwa wa mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi ambaye alikuwa akiukosoa pakubwa utawala wa Aal Saud.  

Saud al Qahtani, mwanzilishi wa kurasa na akaunti bandai dhidi ya wapinzani wa Saudia
 

Mashirika mbalimbali ya kijasusi duniani ikiwemo CIA yameripoti kuwa mauaji hayo yalifanywa kwa amri ya mrithi huyo wa kiti cha ufalme wa Saudia. Khashoggi kwa mara kadhaa alishawahi kuukosoa utawala wa Saudi Arabia kwa kukiuka pakubwa haki za binadamu na kutenda jinai za kivita huko Yemen.