China yaionya Uingereza kuhusu kuchochea ghasia Hong Kong
China imeionya Uingereza na kuitaka iache kuingilia mambo yake ya ndani baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Dominic Raab kutaka uchunguzi huru ufanyike kuhusu ghasia za hivi karibuni katika koloni lake la zamani, Hong Kong.
Katika taarifa, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Hua Chunying amesema kadhia ya Hong Kong ni ya ndani ya China na hivyo Uingereza haipaswi kujiingiza katika suala hilo.
China imekasirishwa na hatua ya Raab kufanya mazungumzo ya simu na Mtendaji Mkuu wa Hong Kong Carrie Lam ambapo alimtaka aruhusu Wahongkong waendelee kuandamana dhidi ya China.
Juzi pia, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China alisema uingiliaji wa mara kwa mara wa Marekani kwenye maswala ya Hong Kong utakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa watu wote wa China ikiwa ni pamoja na wale wa Hong Kong.
Bibi Hua amesema hayo baada ya msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kusema kuwa kitendo cha vyombo nya habari vya China kusambaza taarifa binafsi za ofisa wa ubalozi wake mdogo Hong Kong aliyewasiliana na wahauni wanaoibua ghasia Hong Kong hakikubaliki, na kudai kwamba mkutano kati ya wanadiplomasia wa Marekani na wapinzani wa serikali za nchi nyingine ni wa kawaida.
Mwezi uliopitia katika maadhimisho ya mwaka wa 22 tangu Uingereza kulirudisha jiji la Hong Kong katika mamlaka ya China, waandamanaji wenye misimamo mikali walivamia bunge na kuingia ndani kwa nguvu na kutundika humo bendera ya enzi ya ukoloni wa Uingereza huku wakiwa wamebaba mabango yenye maandishi ya kuipinga China.