China yaionya Marekani kwa kuingilia mambo ya ndani ya Hong Kong
Kwa mara nyingine Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ameionya Marekani kwa hatua yake ya kuingilia masuala ya ndani ya eneo la Hong Kong.
Geng Shuang ameyasema hayo katika radiamali yake kufuatia uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya eneo hilo ambapo ameitaka Washington kuhitimisha mara moja uingiliaji wake katika masuala ya Hong Kong. Hatua hiyo imekuja kufuatia matamshi ya hivi karibuni ya Nancy Pelosi, Spika wa Bunge la Marekani wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na 'mpango wa haki za binaadamu na kidemokrasia mjini Hong Kong kwa mwaka 2019' ambapo aliwaalika kwenye kikao hicho baadhi ya shakhsia wa eneo hilo wanaopigania kujitenga na serikali kuu ya China.
Machafuko na maandamano mjini Hong Kong yaliibuka yapata miezi mitatu iliyopita katika kulalamikia mpango wa kuwarejesha watuhumiwa wa uhalifu katika eneo hilo China. Nchi kama vile Marekani na Uingereza sambamba na kushikilia bango kadhia hiyo, zimekuwa zikichochea moto wa malalamiko hayo mjini Hong Kong. Inafaa kuashiria kuwa, mji huo ulikuwa chini ya udhibiti wa Uingereza tangu mwaka 1842 hadi mwaka 1997. Katika sehemu nyingine Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ameonyesha matumaini yake kuwa kadhia ya kushambuliwa shirika la mafuta la Saudi Arabia ARAMCO itafanyiwa uchunguzi kwa uwazi na uadilifu.