Umoja wa Ulaya wataka faili la mauaji ya Khashoggi lifuatiliwe
Umoja wa Ulaya umetoa taarifa ukisisitiza udharura na umuhimu wa kufuatiliwa faili la mauaji ya mwandishi habari na mkosoaji wa utawala wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi.
Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Ulaya, Maja Kocijančič kwa mnasaba wa kutimia mwaka mmoja tangu Khashoggi alipouawa ndani ya ubalozi wa Saudia mjini Istanbul, imesema kuwa hadi sasa kuna maswali mengi ambayo hayajapewa majibu kuhusiana na mauaji ya kutisha ya mwandishi na mkosoaji huyo wa utawala wa Riyadh.
Taarifa hiyo imesema kuwa, Umoja wa Ulaya unataka kufanyike uchunguzi wa wazi kuhusu mauaji ya Jamal Khashoggi.
Wakati huo huo ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa Agnes Callamard amesema katika kikao kilichofanyika jana mbele ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul, mahala Khashoggi alipouliwa na kukatwa vipande vipande, kwamba matamshi yaliyotolewa siku chache zilizopita na mrithi wa ufalme wa Saudia, Muhammad bin Salman yanathibitisha kwamba Serikali ya Riyadh ilihusika na mauaji ya Jamal Khashoggi.
Callamard amesema uchunguzi huru unaonesha kuwa, kuna ushahidi wa kutosha unaothibitisha kwamba, Bin Salman alihusika na mauaji ya Jamal Khashoggi.
Wanaharakati, jumuiya za kutetea waandishi wa habari na marafiki wa Jamal Khashoggi walikusanyika jana mbele ya ubalozi wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki kukumbuka mauaji ya mkosoaji huyo wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia. Mkutano huo ulihudhuriwa na ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa, Agnes Callamard, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Tawakkol Karman na tajiri mkubwa kuliko wote duniani Jeff Bezos ambaye ndiye mmiliki wa gazeti la Washington Post.
Jamal Khashogi mwandishi wa gazeti la Washington Post tarehe Pili Oktoba 2018 alieleka katika ubalozi wa Saudia mjini Istanbul huko Uturuki kwa ajili ya masuala ya kiidara lakini kamwe hakutoka hai ubalozini humo. Timu ya askari usalama wa Saudi Araba iliyokuwa imetumwa Istanbul kwa kutumia ndege makhsusi ilimuua Jamal Khashoggi ndani ya ubalozi huo na maiti yake ikakatwa vipande vipande.