Kuendelea mkwamo wa Brexit baina ya Uingereza na Umoja wa Ulaya
Mpango wa Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya maarufu kama Brexit umegeuka na kuwa tatizo lisilo na ufumbuzi kwani licha ya mazungumzo kadha wa kadha baina ya viongozi wa serikali ya kihafidhina ya London na maafisa wa Umoja wa Ulaya, lakini bado hakujapatikana njia ya kulipatia ufumbuzi suala hilo.
Katika uwanja huo, David Sassoli, Spika mpya wa Bunge la Ulaya alitangaza Jumanne ya jana baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Boris Johnson, Waziri Mkuu wa Uingereza kwamba: Hakuna hatua yoyote iliyopigwa kuhusiana na Brexit. David Sassoli alisema kuwa, kujiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya bila ya kufikiwa makubaliano na umoja huo kutakuwa na matokeo mabaya na kuongeza kuwa, jambo hilo litakuwa na madhara ya kiuchumi kwa pande zote mbili hususan Uingereza na kuwa na matokeo mabaya kwa Ireland ya Kaskazini.
Spika mpya wa Bunge la Ulaya kadhalika amesema kuwa, matokeo yote mabaya ya kutofikiwa makubaliano ya Brexit yataikumba serikali ya Uingereza. Afisa huyo wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya amesema kuwa, pendekezo la serikali ya Boris Johnson, Waziri Mkuu wa Uingereza si lenye kutekelezeka kivitendo na liko mbali mno na mtazamo wa Bunge la Ulaya na akaongeza kusema kuwa, hawako tayari kukubali pendekezo jipya kwa gharama yoyote ile.
Jumatano iliyopita Boris Johnson aliweka wazi pendekezo jipya la serikali ya Uingereza kuhusiana na namna ya kutekelezwa mpango wa kujiondoa nchi hiyo katika Umoja wa Ulaya (Brexit) na kukabidhi kopi ya mpango huo kwa Umoja wa Ulaya. Katika mpango huo, Boris Johnson amependekeza kuwa, mpango wa backstop kuhusiana na Ireland ya Kaskazini na hali ya mpakani baina ya Ireland Mbili ufutwe katika rasimu ya mpango wa Brexit na badala yake yatekelezwe masuala kama ya kudhibiti mabadilishano ya bidhaa na kufuata kanuni za soko la pamoja la Umoja wa Ulaya.
Kwa utaratibu huo, Ireland ya Kaskazini pamoja na Uingereza zijitoe katika muda uliopangwa yaani 2020 katika Umoja wa Forodha wa Ulaya, lakini iendelee kutii na kufuata sheria na kanuni za soko la pamoja la Umoja wa Ulaya hadi 2025. Donald Tusk, Mkuu wa Baraza la Umoja wa Ulaya ametangaza kuwa, hajakinaika na mpango huo Johnson. Naye Michel Barnier, mjumbe mwandamizi wa Baraza la Ulaya katika masuala ya Brexit anasema kuwa, mpango huo unatofautiana sana na mtazamo wa Umoja wa Ulaya. Suala la mipaka ya Ireland linahesabiwa kuwa ni moja ya changamoto kubwa katika njia ya kujiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya.
Waziri Mkuu wa Uingereza alikuwa na matarajio ya kufanya mazungumzo mapya na Brussels endapo mpango wake ungekubaliwa na hivyo kufikia makubaliano mapya katika kikao cha wakuu wa Umoja wa Ulaya ambacho kimepangwa kufanyika katikati ya mwezi huu wa Oktoba na hivyo makubaliano hayo kupasishwa. Pamoja na hayo, Umoja wa Ulaya umepinga vikali mpango huo wa Johnson na unasisitiza kutekelezwa mpango uliofikiwa kati Umoja wa Ulaya na Theresa May, Waziri Mkuu aliyepita wa Uingereza mpango ambao ulifikiwa Novemba 2018. Si hayo tu, bali viongozi wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya wanaamini kwamba, utendaji wa Waziri Mkuu wa sasa wa Uingereza unahatarisha mustakabali wa Ulaya.
Akizungumza Jumanne ya jana tarehe 8 Oktoba, Donald Tusk, Mkuu wa Baraza la Ulaya alimtuhumu Boris Johnson kwamba, anauchezea mustakabali wa Ulaya. Tusk aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter akimhutubu Johnson kwamba: Suala si kupata ushindi katika mchezo wa kijinga na kila mmoja kumlaumu mwenzake. Filihali, suala la mustakabali wa Ulaya, Uingereza, usalama na maslahi ya mataifa yote ndiyo yaliyopo uwanjani. Wewe hufuatilii suala la kufikiwa makubaliano, hufuatilii suala la kuongezwa muda wa Brexit na wala hufuatilii suala la kufutwa kujitenga, unaelekea wapi?
Ujumbe huo wa Twitter wa Donald Tusk umetolewa ikiwa imebakia wiki moja tu kabla ya kukutana wakuu wa Umoja wa Ulaya ambapo kadhia ya Uingereza kujitoa katika umoja huo inatarajiwa kujadiliwa. Angela Merkel, Kansela wa Ujerumani Jumatatu ya juzi alisema kuwa, kuna uwezekano mkubwa wa kutofikiwa makubaliano kati ya London na Brussels kuhusiana na kujitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya. Matamshi ya Donald Tusk, Mkuu wa Baraza la Ulaya na Angela Merkel, Kansela wa Ujerumani kuhusiana na Brexit yanatolewa katika hali ambayo, wasaidizi wa Boris Johnson wamesema kuwa, mazungumzo ya pande mbili huko Brussels yanakaribia kuvunjika. Uingereza ina muhula wa hadi 2019 iwe imefikia makubaliano na Umoja wa Ulaya kuhusiana na namna ya kujiondoa katika umoja huo au ijitoe bila ya kufikia makubaliano na umoja huo. Pamoja na hayo kuna wasiwasi mkubwa wa matokeo mabaya ndani na nje ya Uingereza endapo nchi hiyo itajiondoa katika Umoja wa Ulaya bila ya kufikia makubaliano.