UN yataka kufunguliwa kesi ya jinai zinazofanywa dhidi ya Waislamu Myanmar
Maafisa wawili wa Umoja wa Mataifa wametoa wito wa kufunguliwa kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ili kushughulikia jinai zinazofanywa na jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya katika jimbo la Rakhine nchini humo.
Wito huo umetolewa na ripota maalumu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Myanmar, Yanghee Lee na na Mwenyekiti wa Kamisheni Huru ya Kutafuta Ukweli kuhusu Myanmar, Marzuki Darusman katika mkutano wa waandishi wa habari mjini New York.
Yanghee Lee ametoa wito wa kuwekwa vikwazo dhidi ya makampuni yanayomilikiwa na jeshi la Myanmar na makamanda wa jeshi waliohusika na jinai kubwa dhidi ya binadamu na jinai za kivita dhidi ya Waislamu wa Rohingya.
Ripota huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema hali ya haki za binadamu nchini Myanmar haijaboreka tangu mwaka 2017 na ubaguzi dhidi ya Waislamu unaendelea bila ya kusita katika eneo la Rakhine na katika mji mkuu wa nchi hiyo ambako zaidi ya Waislamu laki moja na 20 elfu wa jamii ya Rohingya wanashikiliwa katika makambi maalumu.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa pia amesema anaamini kuwa, hali ya sasa nchini Myanmar hairuhusu wakimbizi wa jamii ya Rohingya waliokimbilia nje ya nchi kurejea nchini kwao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamisheni Huru ya Kutafuta Ukweli kuhusu Myanmar, Marzuki Darusman ametahadharisha kuhusu hatari kubwa ya mauaji ya kimbari inayowakabili zaidi ya Waislamu laki sita waliobakia Myanmar.
Darusman amesema kuwa, hali ya Waislamu katika jimbo la Rakhine huko Myanmar imekuwa mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa miaka miwili iliyopita.