Kukubali Umoja wa Ulaya kurefusha muhula wa Brexit
Kufuatia Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson kuwasilisha barua ya kutaka kuongezwa muhula wa kujitoa nchi hiyo katika Umoja wa Ulaya, mabalozi wa umoja huo wametangaza kukubali kuongezwa muda huo wa Brexit, lakini bila ya kutaja tarehe maalumu.
Mina Andrew Msemaji wa Kamisheni ya Ulaya amesema baada ya kumalizika kikao cha mabalozi wa umoja huo kwamba, wajumbe wa nchi 27 za Ulaya na mataifa mengine wameafiki masharti ya urefushaji muda wa Brexit na kwa utaratibu huo, nchi za Ulaya zinapaswa ziainishe na kutangaza muhula mpya wa kujitoa Uingereza ndani ya EU.
Nchi wananchama wa Umoja wa Ulaya (EU) zimeitisha kikao ambapo Boris Johnson Waziri Mkuu wa Uingereza ameziomba nchi za umoja huo ziongeze muda wa kujitoa nchi yake katika Umoja wa Ulaya kutokana na mashinikizo ya bunge yanayomkabili na licha ya yeye mwenyewe kuliandikia barua Baraza la Ulaya kuhusu suala hilo. Mswada mkuu wa Brexit uliidhinishwa Jumanne iliyopita katika bunge la Uingereza kwa tofauti ya kura 30, hata hivyo mswada ulioainishwa na serikali kwa ajili ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya umeshindwa kuungwa mkono kwa kura zilizohitajika hadi kufikia mwezi huu.
Hivi sasa mijadala imepamba moto kati ya bunge la Uingereza na serikali kuhusu Brexit; huku Johnson akitishia kuitisha uchaguzi wa kabla ya wakati na kutekeleza Brexit bila ya kufikia mapatano. Kwa kadiri kwamba Waziri Mkuu huyo wa Uingereza baada ya kura hiyo ya bunge alifanya mazungumzo ya simu na Donald Tusk Mwenyekiti wa Baraza la Ulaya na bi Angela Merkel Kansela wa Ujerumani na kueleza kuwa, msimamo wa serikali ni kwamba lazima Uingereza itoke katika Umoja wa Ulaya ifikapo Oktoba 31 mwaka huu licha ya London kutaka kuakhirishwa mchakato huo. Msemaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza amesema kuhusu suala hilo kuwa: "Johnson ametangaza wazi kuwa kuakhirisha kujitoa nchi hiyo ndani ya Umoja wa Ulaya hakutakuwa kwa maslahi ya pande mbili."
Hii ni katika hali ambayo bunge la Uingereza linataka kuongezwa muda wa Brexit ili kuchunguza mapatano yaliyofikiwa; na linaona mazungumzo mapya huenda yakawa bora kwa ajili ya kufikiwa makubaliano. Katika mazingira hayo, barua ya Boris Johnson akiomba kurefushwa muhula wa Brexit imezipelekea nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuitisha kikao cha kuchunguza ombi hilo la London. Hii ni katika hali ambayo awali nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ziliweka wazi kwamba hazitarefusha muda huo tajwa. Aidha kushadidi mgogoro wa Brexit kumemfanya Donald Tusk Mkuu wa Baraza la Ulaya awaombe wakuu wa Ulaya waafiki pendekezo la serikali ya Uingereza kwa ajili ya kuakhirisha mchakato huo wa Brexit.
Hata kama Umoja wa Ulaya umeafiki ombi la kurefushwa muhula wa Brexit lakini jambo hilo limezidisha hitilafu za kimitazamo kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya. Baadhi ya nchi hizo ikiwemo Ufaransa zinataka Uingereze ipatiwe muda wa wiki mbili ili kutekeleza Brexit. Kuhusiana na suala hilo, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ameitaka Uingereza itoke Umoja wa Ulaya katika kipindi cha chini ya wiki mbili; hata hivyo baadhi ya nchi kama Ujerumani na Ireland zimeafiki London iongezewe muda wa miezi mitatu.
"Michel Barnier Mjumbe wa baraza la Ulaya anayehusika na Brexit amesema kuhusiana na suala hilo kwamba: Wakuu wa nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya ndio wenye maamuzi kuhusu kutoa muhula zaidi kwa ajili ya kutekeleza Brexit na Mwenyekiti wa Baraza la Ulaya anafanya mashauriano kuhusu suala hilo."
Upo uwezekano uchaguzi wa bunge nchini Uingereza ukafanyika kabla ya Sikukuu ya Krismasi iwapo Umoja wa Ulaya utaafiki kuakhirisha Brexit hadi kufikia mwishoni mwa Januari 2020; chaguo ambalo haliungwi mkono na wanasiasa nchini humo na ambalo litalifanya kuwa gumu zaidi suala la Brexit. Aidha iwapo London itapewa muda mfupi basi suala hilo linazidisha uwezekano wa kutekelezwa Brexit bila ya mapatano kama anavyotaka Johson mwenyewe. Inaonekana kuwa Umoja wa Ulaya na Uingereza zinazidi kuzongwa na siku za mashaka na hali ngumu kuhusiana na Brexit.