China: Tutakabiliana na wanaotaka kujitenga jimbo la Hong Kong
Naibu Waziri Mkuu wa China ametoa onyo kali kwa kusema kamwe serikali ya nchi hiyo haitovumilia harakati za kujitenga eneo la Hong Kong.
Hyun-jung, ameyasema hayo alipokutana na Carrie Lam, kiongozi wa eneo la Hong Kong mjini Beijing na kusisitiza kwamba hakuna nchi duniani itakayokubali kuvumilia ukatili, uharibifu, uasi na machafuko na kwamba serikali ya China pia haiepukani na jambo hilo. Naibu Waziri Mkuu wa China ameitaka mihimili mitatu ya uongozi kuanzia serikali kuu, vyombo vya mahkama na bunge eneo la Hong Kong, kushirikiana pamoja katika juhudi zenye lengo la kuhitimisha mgogoro wa sasa na kurejesha hali ya uthabiti.
Kabla ya kikao hicho Rais Xi Jinping wa China pia alikutana na Carrie Lam, kiongozi wa eneo la Hong Kong ambapo alimtaka mwanamama huyo kufanya juhudi ili kuhitimisha machafuko katika eneo tajwa. Machafuko na ghasia katika eneo la Hong Kong vilianza zaidi ya miezi minne iliyopita katika kulalamikia muswada wa kuwaondoa wahalifu wa eneo hilo na kuwapeleka kuhukumiwa na serikali ya China. Hata hivyo mataifa kama vile Marekani na Uingereza yamekuwa yakichochea ghasia ndani ya eneo hilo kupitia kuunga mkono suala hilo.