Watoto 700 wanalala katika barabara za mitaa ya Paris, Ufaransa
(last modified Thu, 21 Nov 2019 06:56:29 GMT )
Nov 21, 2019 06:56 UTC
  • Watoto 700 wanalala katika barabara za mitaa ya Paris, Ufaransa

Jumuiya 12 zinazojihusisha na watoto wasiokuwa na makazi nchini Ufaransa zimefichua kwamba, watoto wadogo 700 wanaishi pamoja na familia zao katika barabara za mitaa ya mji mkuu wa nchi hiyo, Paris.

Jumuiya hizo zimetangaza kuwa, zimeomba serikali ya Ufaransa ianzishe haraka kituo cha kuwahifadhi watoto hao wanaolazimika kulala barabarani kutokana na kukosa makazi.

Taarifa iliyotolewa na jumuiya hizo imesema kuwa, watoto 700 wanaishi pamoja na familia zao katika barabara za Paris na viunga vyake na kwamba watoto wengine elfu 20 wenye umri wa chini ya miaka 18 wanaishi katika vituo vya muda. Taarifa hiyo imesisitiza kuwa hali hii haikubaliki kwa nchi kama Ufaransa.

Jumuiya ya "Maiti Mitaani" inayofanya uchunguzi kuhusu watu wasio na makazi nchini Ufaransa imetangaza kuwa watoto 8 kati ya wale wanaolala barabarani pamoja na familia zao wameaga dunia tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

Mamia ya watoto wanalala barabarani Paris

Uchunguzi uliofanywa mwaka jana na Halmashauri ya Jiji la Paris ulibaini kuwa, karibu watu elfu tatu wanalazimika kulala barabarani katika mji huo. Takwimu hizo zilitolewa baada ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kutangaza mwaka wa 2017 kwamba hakuna mtu atakayelazimika kulala barabarani ncini Ufaransa hadi mwishoni mwa mwaka huo.