Mlipuko wa ugonjwa wa surua waua watu 70 Samoa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i57784-mlipuko_wa_ugonjwa_wa_surua_waua_watu_70_samoa
Umoja wa Mataifa umesema mlipuko wa ugonjwa wa surua (measles) umeua makumi ya watu katika kisiwa cha Samoa kilichoko katika Bahari ya Pacific.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 10, 2019 04:07 UTC
  • Mlipuko wa ugonjwa wa surua waua watu 70 Samoa

Umoja wa Mataifa umesema mlipuko wa ugonjwa wa surua (measles) umeua makumi ya watu katika kisiwa cha Samoa kilichoko katika Bahari ya Pacific.

Mshirikishi wa masuala ya kibinadamu katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mark Lowcock amesema mripuko mpya wa ugonjwa huo umeua watu 70 katika kisiwa hicho ndani ya siku chache zilizopita.

Ameongeza kuwa, kufikia jana asubuhi, kesi mpya 112 za ugonjwa huo zilikuwa zimeripotiwa ndani ya masaa 24. UN imesema kati ya vifo 70 vilivyoripotiwa hadi sasa, 60 ni watoto wadogo walio chini ya umri wa miaka minne. 

Afisa huyo wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa amesema UN imetoa dola milioni 2.6 kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo.

 

Asilimia 90 ya watu 200,000 wa kisiwa cha Samoa wapewa chanjo ya surua

Tangu mripuko wa ugonjwa huo wa ukambi uripotiwe katikati ya mwezi Oktoba mwaka huu katika kisiwa hicho chenye watu laki mbili, kesi  4,693 zimenakiliwa, huku watoto 16 wakiwa miongoni mwa watu 229 waliolazwa hospitalini wakiwa katika hali mbaya.

Hivi karibuni pia, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia watoto (UNICEF) lilisema watu 4,000 wamepoteza maisha tangu mwezi Januari mwaka huu kutokana na ugonjwa huo wa surua na kwamba idadi hiyo ni kati ya wagonjwa 203,179 walioripotiwa kwenye majimbo yote 26 ya taifa hilo.