Dec 11, 2019 01:13 UTC
  • ICJ yaanza kusikiliza kesi kuhusu mauaji ya kimbari ya Waislamu Myanmar

Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) imeanza kusikiliza kesi kuhusu mauaji ya kimbari ya Waislamu wa Myanmar kufuatia shtaka ambalo limewasilishwa na Gambia.

Kesi hiyo, ambayo imeanza Jumanne huko The Hague,  ni hatua ya kwanza ya kisheria ya kuwafikisha kizimbani watawala wa Myanmar ambao wamehusika na jinai dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya.

Gambia, ambayo imewasilisha kesi hiyo kwa niaba ya nchi 57 wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), imetoa wito kwa ICJ kuchukua hatua za dharura kusitisha vitendo vya Myanmar vya mauaji ya kimbari dhidi ya Warohingya.

Akizungumza katika kikao cha mahakama, Waziri wa Sheria wa Gambia Abubacarr Tambadou amesema: "Kile ambacho Gambia inaomba ni kuwa, muitake Myanmar isitishe mauaji na ukatili ambao unaendelea na isimamishe mauaji ya kimbari dhidi ya watu wake."

Waislamu wa jamii ya Rohingya wakisaka hifadhi baada ya makazi yao kuteketezwa moto katika kampeni ya mauaji ya kimbari nchini Myanmar

 Mwezi uliopita, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema bado anaendelea kuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya Myanmar, likiwemo jimbo la Rakhine kutokana na kukandamizwa Waislamu wa jamii ya Rohingya katika eneo hilo.

Ikumbukwe kuwa, Agosti 25 mwaka 2017 Waislamu wapatao 740,000 wa jamii ya Rohingya walilazimika kuyahama makazi yao kwa umati katika jimbo lao la Rakhine na kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh walikojiunga na wenzao wengine laki mbili waliokuweko nchini humo, baada ya vikosi vya jeshi la Myanmar na Mabudhha wenye misimamo ya kufurutu ada kuanzisha wimbi kubwa la hujuma na ukandamizaji dhidi ya Waislamu hao.

Aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein aliesema kuwa uhalifu unaofanywa na Mabudha kwa himaya ya serikali nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ni mauaji ya kimbari.

 

Tags