Dec 16, 2019 12:12 UTC
  • Maelfu ya watu wasio na makazi wamefariki dunia mjini London

Vyombo vya habari nchini Uingereza vimetangaza habari ya kufariki dunia maelfu ya watu wasio na makazi mjini London, mji mkuu wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, jumla ya watu elfu tatu wamepoteza maisha kwa kukosa makazi mjini London pekee katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Aidha takwimu hiyo iliyotolewa na asasi za misaada imeonyesha kwamba hadi sasa karibu watu laki tatu na elfu 20 hawana makazi nchini Uingereza wakiwemo watu laki moja na elfu 70 wanaoishi mjini London. Asasi za misaada ya kibinaadamu nchini Uingereza pia zimetangaza kwamba, karibu watu elfu tano hawana mahala popote pa kujihifadhi ambapo majira ya usiku hulala barabarani hadi asubuhi.

Malaki ya watu wanalala nje nchini Uingereza, huku nchi hiyo ikizikosoa nchi masikini duniani kuhusu suala hilo

Tarehe saba ya mwezi huu kundi moja la wakazi wa mji wa London kwa lengo la kutangaza mshikamano wake na watu wasio na makazi mjini humo, lililala katika barabara za medani ya Trafalgar ya katikati mwa mji huo. Hatua hiyo ilibuniwa na kundi moja la kujitolea kwa ajili ya kukusanya misaada ya kifedha ili kuwasaidia watu wasio na makazi kote duniani. Matatizo ya kiuchumi ambayo yameikumba Uingereza katika miaka ya hivi karibuni, yamebadilisha mfumo wa maisha ya wananchi na kuwalazimisha wengine kukimbia makazi yao kutokana na kushindwa kumudu gharama za kupangisha nyumba au kutokana na kudaiwa na benki.

Tags