Mwakilishi wa Iran UN: Marekani iondoke magharibi mwa Asia
Balozi na mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, Luteni Jenerali shahidi Qassem Soleimani ni shujaa wa mapambano dhidi ya ugaidi katika eneo la magharibi mwa Asia na kuongeza kuwa, Marekani inapaswa kuondoka katika eneo hilo.
Katika mazungumzo yake na televisheni ya al Jazeera ya Qatar, Majid Takht-Ravanchi ameashiria mauaji ya kigaidi yaliyofanywa na Marekani dhidi ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) huko Baghdad nchini Iraq na kusema: Rais Donald Trump wa Marekani alipewa ushauri mbaya na kuchukua maamuzi yasiyo sahihi ya kumuua kigaidi Shahidi Soleimani.
Takht-Ravanchi amesema kuwa jibu la Iran kwa mashambulizi ya kigaidi ya Marekani lilitolewa kwa kutegemea sheria ya kimataifa ya haki ya kujihami na kusisitiza kuwa: Iwapo Marekani itafanya kosa jingine, Iran haitakaa kimya kama mtazamaji tu, na itatoa jibu tofauti kabisa.
Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa azimio la Bunge la Iraq la kuwafukuza askari wa Marekani katika ardhi ya nchi hiyo ni matokeo ya uvamizi wa zaidi ya miaka 17 wa Wamarekani nchini Iraq. Amesema kuwa utendaji na mienendo ya Marekani haikubaliki na kuongeza kuwa, Iran na nchi za magharibi mwa Asia zinaweza kutatua matatizo yao bila ya uingiliaji kati wa Marekani.
Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC, Ijumaa Alfajiri 3 Januari aliwasili nchini Iraq kufuatia mwaliko rasmi wa wakuu wa nchi hiyo. Punde baada ya kuwasili, akiwa ndani ya gari pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Kamanda wa kikosi cha kujitolea cha wananchi wa Iraq maarufu kama al Hashd al Shaabi pamoja na watu wengine wanane, walishambuliwa tokea angani na wanajeshi vamizi na magaidi wa Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad na wakaua shahidi katika tukio hilo.