Ripota Maalumu wa UN: Mauaji ya Soleimani yalikiuka sheria za kimataifa
Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa amesema mauaji ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani, kamanda shahidi wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) yalikiuka sheria za kimataifa na Hati ya UN.
Agnès Callamard amesema hayo katika ripoti yake juu ya mauaji hayo ya kigaidi na kubainisha kuwa, Marekani imeshindwa kutoa ushahidi wa kutosha wa kuyapa nguvu madai yake kwamba Jenerali Soleimani alikuwa tishio kwa taifa hilo.
Mtaalamu huyo wa ngazi za juu wa UN ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, "dunia hivi sasa ipo katika kipindi nyeti cha kutizamwa upya matumizi ya droni. Hata hivyo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halijachukua hatua yoyote huku jamii ya kimataifa kwa kujua au kutojua imeendelea kunyamaza kimya."
Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa ambaye Alkhamisi ijayo anapaswa kuwasilisha faili la mauaji hayo mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la UN amesema: "mauaji ya kigaidi ya Jenerali Qassem Soleimani yalikanyaga kikamilifu vigezo vinavyohusiana na nchi kutumia nguvu za kijeshi nje ya mipaka yake."

Wiki iliyopita, Mwendesha Mashtaka wa Tehran alitoa waranti wa kutiwa mbaroni watu 36 akiwemo Rais Donald Trump wa Marekani wakihusishwa na mauaji ya Shahid Qassem Soleimani. Mwendesha Mashtaka wa Tehran alieleza kuwa, tayari wameitaka Polisi ya Kimataifa Interpol kuwatia mbaroni wahalifu hao.
Itakumbukwa kuwa, tarehe 3 Januari mwaka huu, jeshi la kigaidi la Marekani kwa amri ya rais wa nchi hiyo Donald Trump lilimuua kidhulma Luteni Jenerali Qassem Soleimani akiwa uraiani nchini Iraq tena akiwa mgeni rasmi wa serikali ya Baghdad.
Nchi nyingi duniani, mashirika, taasisi na makundi mbalimbali yalilaani vikali mauaji hayo ya kigaidi yaliyofanywa na Marekani dhidi ya kamanda huyo shujaa aliyekuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya magenge ya kigaidi katika eneo la Asia Magharibi.