Sep 14, 2020 08:41 UTC
  • Antje Jackelén
    Antje Jackelén

Askofu Mkuu wa Sweden na maafisa wengine wa ngazi za juu wa kanisa la nchi hiyo wametoa taarifa wakilaani kitendo cha kundi moja lenye misimamo mikali la nchi hiyo cha kuivunjia heshima Qur'ani tukufu.

Hayo yameelezwa katika taarifa iliyotolewa na Baraza la Kikristo la Sweden ambalo limelaani vikali hatua ya chama cha mrengo wa kulia cha Hard Line ya kukivunjia heshima kitabu kitukufu cha Qur'ani. 

Katika taarifa hiyo wachungaji kumi wa ngazi za juu wa Kanisa la Protestanti la Sweden wakiongozwa na Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Antje Jackelén wamelaani hujuma inayolenga matukufu na itikadi za Waislamu. 

Askofu Mkuu Antje Jackelén amesema viongozi wa kidini wa Sweden wananajitenga kikamilifu na kitendo hicho cha kuvunjia heshima kwa makudusi itikadi za wafuasi wa dini nyingine.

Taarifa ya viongozi hao wa Kanisa la Protestanti nchini Sweden imesema kuwa  kuvunjia heshima kitabu cha Qur'ani ni kitendo cha kihayawani. 

Alkhamisi iliyopita mjumbe wa chama chenye misimamo mikali cha Hard Line nchini Denmark alikivujia heshima kitabu kitakatifu cha Qur'ani kwa kuchoma moto nakala ya kitabu hicho katika kitongoji cha wabaguzi wa rangi cha Rinkeby mjini Stockholm.

Uhalifu huo umefanyika siku kadhaa baada ya chama cha mrengo wa kulia cha Hard Line nchini Denmark kuhujumu dini tukufu ya Uislamu katika ukurasa wake wa Facebook. 

Kiongozi wa chama hicho, Rasmus Paludan ambaye pia amewahujumu Waislamu na dini yao, ametoa wito wa kufanyika mandamano dhidi ya Uislamu mjini Stockholm. 

Tarehe 28 mwezi uliopita wa Agosti pia kundi lenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia la Sweden liliitisha maandamano haramu katika mji wa Malmo na kuchoma moto nakala ya kitabu kitukufu cha Qur'ani. 

Miezi ya hivi karibuni nchi za Sweden na Denmark zimeshuhudia hujuma na mashambulizi kadhaa dhidi ya Waislamu na maeneo yao ya kidini. 

Sambamba na hujuma hiyo dhidi ya matukufu ya Kiislamu katika nchi za Sweden na Denmark, jarida la Kifaransa la Charlie Hebdo Jumatano iliyopita, lilichapisha vibonzo vinavyomkebehi na kumvunjia heshima Mtume wa mwisho wa Mwenyezi, Muhammad (saw).

Tags