Tatizo la uwepo wa magaidi wa kitakfiri katika mzozo wa Karabakh
(last modified Mon, 09 Nov 2020 11:22:12 GMT )
Nov 09, 2020 11:22 UTC
  • Tatizo la uwepo wa magaidi wa kitakfiri katika mzozo wa Karabakh

Uwepo wa magaidi wa kitakfiri katika eneo linalogombaniwa la Nagorno Karabakh unaendelea kubadilika taratibu na kuwa tatizo kubwa kwa serikali za eneo.

Katika hali ambayo viongozi wa Azerbaijan akiwemo Rais Ilham Aliyev, wanakanusha kuwepo kwa hata askari mmoja wa kigeni huko Karabakh, lakini viongozi wa Armenia na Russia wanaendelea kuelezea wasiwasi wao kuhusu suala hilo. Kwa mfano, akizungumza karibuni na gazeti la Kommersant linalochapishwa mjini Moscow, Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema: Magaidi wa kigeni ambao wamehamia Karabakh kutokea Asia Magharibi wanapata 2000.

Katika uwanja huo huo Bi. Maria Zakharova, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amezungumza na waandishi habari na kuonya kwa kusema: Kuhamishiwa magaidi huko Karabakh kutoka Asia Magharibi kunaweza kuwafanya wadhibiti eneo zima la kusini mwa Caucasia.

Ni wazi kuwa kuhamishiwa magaidi katika eneo lililotajwa kunaweza kuwa na taathira hasi kwa nchi huru za eneo hilo. Mbali na hayo suala hilo linaweza pia kuhatarisha usalama wa mipaka ya nchi zote za Asia ya Kati na Caucasia Kusini. Pamoja na hayo, suala la kuhamishiwa magaidi katika eneo hilo sio jambo geni.

Sergey Lavrov

Kabla ya hapo Marekani ilifanya juhudi kubwa za kutuma manambamgo wa kigaidi katika mipaka ya Afghanistan na nchi za Asia ya Kati. Kuhamishwa magaidi wa kitakfiri kutoka Syria kwenda mipaka ya nchi za Caucasia Kusini ni jambo linalokwenda sambamba na siasa za kujiimarisha Marekani katika mipaka ya Russia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Utawala haramu wa Israel pia unaweza kunufaika na jambo hilo. Uzeofu wa miongo iliyopita unathibitisha wazi kwamba kuenea machafuko katika eneo hilo ni kwa manufaa na malengo ya Marekani na utawala ghasibu wa Israel.

Katika uwanja huo, Subhan Muhaqiq anasema: Iwapo itathibiti kwamba Uturuki inahamisha magaidi wa kitakfiri na wasio wa kitakfiri kutoka Syria na Libya na kuwapeleka Karabakh, ni wazi kuwa katika siku chache zijazo kwa mara nyingine tena kutatokea makabiliano kati ya Moscow na Ankara. Na hasa ikitiliwa maanani kwamba hatua hiyo inahatarisha moja kwa moja usalama wa Russia.

Huenda ni kutokana na ukweli huo ndipo katika mojawapo ya vipekee vya mapendekezo ya Iran ya kusuluhisha mgogoro wa Karabakh suala hilo la usalama wa nchi jirani likaashiriwa moja kwa moja na kupewa uzito mkubwa. Kwa vyovyote vile tunapasa kusema kuwa maonyo ya viongozi wa Russia kuhusiana na kutumwa magaidi wa kitakfiri katika eneo la Karabakh kutoka Syria yanatolewa katika hali ambayo hivi karibuni Rais Bashar al-Asad wa Syria pia alithibitisha kuwa Uturuki inatuma askari hao huko Karabakh kutoka nchini kwake.

Athari za mapigano katika eneo la Karabakh

Bashar al-Asad alimkosoa Rais Recep Erdogan wa Uturuki kwa kuanzisha mgogoro wa Karabakh kwa kusema: Uturuki inawatumia magaidi ambao inawakusanya kutoka Syria na nchi nyingine katika mapigano yanayoendelea kati ya Azerbaijan na Armenia katika mgogoro wa Karabakh.

Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, hatua ya Uturuki kutuma na kuwatumia magaidi katika eneo la Caucasia ni katika kudumisha mkondo ule ule wa siasa za kibeberu za Marekani katika eneo. Kwa kutuma magaidi 2000 huko Caucasia Kusini, kwa hakika Uturuki imeisaidia Marekani katika kupunguza ukosoaji na lawama ambazo zimekuwa zikitolewa dhidi yake na serikali pamoja na wataalamu wa eneo la Asia Kusini na Caucasia katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Bila shaka siasa hizo pia zimezisaidia Marekani na utawala wa Kizayuni kupunguza gharama ya kutuma magaidi hao kutoka Syria hadi karibu na mipaka ya Russia, bila ya kuamsha hasira na ukosoaji wa moja kwa moja wa wataalamu wa masuala ya kisiasa na kiusalama katika eneo.