Obama: Mienendo na rekodi ya Trump ichunguzwe
https://parstoday.ir/sw/news/world-i6565-obama_mienendo_na_rekodi_ya_trump_ichunguzwe
Rais Barack Obama wa Marekani ametoa wito wa kutathminiwa na kuchunguzwa mienendo ya sasa na ya huko nyuma ya Donald Trump, mwanasiasa anayetaka kuchaguliwa kuwania urais nchini humo kupitia chama cha Republican.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 07, 2016 07:26 UTC
  • Obama: Mienendo na rekodi ya Trump ichunguzwe

Rais Barack Obama wa Marekani ametoa wito wa kutathminiwa na kuchunguzwa mienendo ya sasa na ya huko nyuma ya Donald Trump, mwanasiasa anayetaka kuchaguliwa kuwania urais nchini humo kupitia chama cha Republican.

Akizungumza kwa mara ya kwanza hadharani juu ya msimamo wake kwa Trump jana Ijumaa katika Ikulu ya White House mjini Washington, Obama alisema matamshi ya mwanasiasa huyo yanafaa kuchukuliwa kwa uzito na kuwekwa kwenye mizani ili Wamarekani wapime iwapo anafaa kuwa rais au hafai.

Obama amesema kauli za Trump haswa katika maswala ya usalama wa taifa na sera za kigeni ni za kutiliwa shaka na kusisitiza kuwa: "Urais hapa nchini sio mchezo wa kuigiza."

kadhalika Rais wa Marekani amevitaka vyombo vya habari kutoangazia tu kile alichokitaja kuwa kauli za kisanii za mwanasiasa huyo bali viangazie pia matamshi yake ambayo yanaweza kuzusha vita, kutia doa uhusiano wa Washington na nchi zingine na kuvuruga mfumo wa uchumi wa Marekani. Weledi wa sera za kigeni na usalama Marekani na hata wanasiasa wa chama cha Republican wameonya kuhusu mitazamo ya kufurutu ada ya Trump. Wanasema matamshi ya chuki na kibaguzi ya Trump si tu kuwa yanahatarisha usalama wa Marekani pekee bali wa dunia nzima kwa ujumla.