Mar 11, 2021 00:48 UTC
  • Wasiwasi kuhusu vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu nchini Uswisi

Kuenea chuki dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi na hasa barani Ulaya katika miaka ya karibuni kumeibua matukio na radiamali tofauti.

Hatua ya karibuni kabisa katika uwanja huo ni kufanyika kura ya maoni kwa ajili ya kupiga marufuku vazi la burqa katika nchi ya Uswisi, jambo ambalo limeibua radiamali hasi kutoka kwa mashirika na jumuiya tofauti za Kiislamu. Jumuiya za Kiislamu nchini Uswisi huku zikitangaza 'siku nyeusi' kwa Waislamu zimesema kuwa marufuku hiyo dhidi ya vazi la hijabu la burqa ni aina fulani ya ubaguzi dhidi ya wanawake. Wanawake wengi wa Kiislamu wa Uswisi pia wamelaani kura hiyo ya maoni na kusisitiza kuwa uvaaji wao wa burqa ni uamuzi wa mtu binafsi na wala sio tangazo kwa ulimwengu wa nje.

Akifafanua suala hilo, Anis El Sheikh, msemaji wa kundi la wanawake wa Kiislamu wanaounga mkono wanawake wanaovalia mitandio amesema kuwa licha ya kwamba sheria hiyo ya kupiga marufuku burqa haina faida yoyote lakini pia ni alama ya ubaguzi wa rangi.

Kampeni za chuki dhidi ya vazi la wanawake wa Kiislamu

Katika kura ya maoni iliyofanyika Jumapili tarehe 7 Machi, raia wa Uswisi waliunga mkono marufuku dhidi ya uvaaji wa burqa katika maeneo ya umma. Kwa mujibu wa matokeo ya kura hiyo, asilimia 52 ya walioshiriki katika kura hiyo waliunga mkono marufuku hiyo na wengine asilimia 48 wakapinga. Marufuku hiyo ina maana kuwa kuanzia sasa hakuna mwanamke yeyote nchini Uswisi atakayeruhusiwa kuufunika uso wake wote anapokuwa katika maeneo ya umma. Pendekezo la kufanyika kura hiyo ya maoni lilitolewa na chama cha mrengo wa kulia cha SVP, ambacho katika muongo mmoja uliopita kimekuwa kikiendesha kampeni kali za chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu ikiwemo ya kupiga marufuku ujenzi wa minara kwenye misikiti.

Hata kama chama hicho hakikuashiria burqa moja kwa moja katika pendekezo la kura hiyo ya maoni lakini ni wazi kuwa wanawake wa Kiislamu ndio waliolegwa kwenye pendekezo hilo. Hii ni kutokana na kuwa nara za chuki dhidi ya Uislamu kama vile 'simamisheni Uslamu wenye misimamo mikali' na 'simamisheni uchupaji mipaka' zilizoandamana na picha ya mwanamke wa Kiislamu aliyevalia burqa nyeusi ziliwakusudia Waislamu. Katika upande wa pili wapinzani wa kura hiyo ya maoni walibeba mabango yaliyokuwa yameandikwa nara za kupinga marufuku hiyo iliyo dhidi ya Uislamu na kusema kuwa haina faida yoyote kwa Uswisi. Kwa upande wake serikali ya Uswisi ilipinga kura hiyo ya maoni si kwa kuwa inapingana na uhuru wa kujieleza na haki za binadamu bali kwa kuwa haikuwa na manufaa yoyote kwa taifa la Uswisi. Ilisema kuwa hilo halikuwa tatizo kuu la Uswisi kwa sasa bali huenda likadhuru sekta ya utalii ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Nasrullah Tajik, mtaalamu wa masuala ya kisiasa, mambo yamebadilika kiasi kwamba kama kuna wakati ambao Waislamu walihisi kuwa na usalama wa kiwango fulani katika nchi za Magharibi, sasa hali hiyo imebadilika na hawahisi tena kuwa salama na daima wako chini ya mashinikizo ya chuki dhidi ya Uislamu.

Waislamu wa Uswisi waandamana kutetea imani na haki zao

Kabla ya hapo nchi nyingine za Ulaya kama Austria, Uholanzi, Ubelgiji, Ujerumani, Bulgaria na Ufaransa zilizikuwa tayari zimepiga marufuku burqa. Ufaransa ambayo inaoongoza miongoni mwa nchi za Ulaya katika kueneza chuki dhidi ya Uislamu ilikuwa nchi ya kwanza barani humo kupitisha sheria ya kupinga wanawake wa Kiislamu kufunika nyuso zao mwaka 2011. Pamoja na hayo sheria hiyo ilipingwa mwaka 2014 na Mahakama ya Haki za Binadamu ya Ulaya kwa msingi kuwa ilikuwa inakiuka wazi sheria ya uhuru wa mavazi ya kidini. Katika miaka kadhaa iliyopita mamia ya wanawake wa Kiislamu wametiwa nguvuni na kupigwa faini nchini Ufaransa kwa madai ya kukiuka sheria hiyo. Kwa hakika Waislamu wengi barani Ulaya wanapitia hali ngumu ya mateso, ubaguzi na chuki dhidi ya dini. Kwa ujumla mazingira yamekuwa magumu kwa Waislamu wanaoishi katika nchi za Ulaya kutokana na wimbi kubwa la chuki na propaganda hasi zinazoenezwa na vyombo vya habari vya nchi hizo dhidi ya Uislamu na Waislamu. Kichekesho ni kwamba wanaoeneza siasa hizo chafu wanadai kuwa katika mstari wa mbele wa kutetea uhuru, demokrasia na haki za binadamu duniani.

Tags