Ulyanov: Lengo la mazungumzo ya Vienna ni kuhuisha mapatano ya JCPOA
Mwakilishi wa Russia katika taasisi za kimataifa zenye makao huko Vienna nchini Austria kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa, lengo la mazungumzo ya Vienna ni kuhuisha mapatano ya JCPOA.
Mikhail Ulyanov amesisitiza kuwa, lengo la mazungumzo ya Vienna ni kuhuisha tu mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kuongeza kuwa, pande zote katika mapatano hayo zinapasa kufuatilia lengo hilo la pamoja.
Mazungumzo ya JCPOA yamekaribia awamu ya mwisho baada ya kufanyika duru sita za mazungumzo mapana na mfululizo huko Vienna. Hata hivyo tarehe ya kufanyika duru ijayo ya mauzngumzo hayo bado haijatangazwa.
Timu za mazungumzo hayo zimeeleza kufurahishwa na hatua zilizopigwa hadi sasa kwa lengo la kufufua mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kusisitiza tena azma yao ya ya kufuatilia mchakato wa mazungumzo hayo kwa lengo la kupata njia za ufumbuzi wa masuala yaliyosalia.
Serikali mpya ya Marekani chini ya uongozi wa Rais Joe Biden imekiri kufeli sera za mashinikizo ya kiwango cha juu za serikali ya kabla yake dhidi ya Iran. Biden ametangaza kuwa anataraji kuirejesha Washington katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA lakini hadi sasa hajachukua hatua ya maana kuhusu suala hilo.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa upande wake imesisitiza kuwa, itatekeleza tena majukumu yake kwa mujibu wa mapatano hayo ya nyuklia pale Marekani nayo itakapoiondolea nchi hii vikwazo na kujiridhisha na hatua hiyo.