Russia: Mazungumzo ya nyuklia ya JCPOA yataanza tena karibuni mjini Vienna
(last modified Sat, 21 Aug 2021 12:46:25 GMT )
Aug 21, 2021 12:46 UTC
  • Russia: Mazungumzo ya nyuklia ya JCPOA yataanza tena karibuni mjini Vienna

Mwakilishi wa Russia katika mashirika ya kimataifa yenye makao yao Vienna amejibu madai yaliyotolewa na afisa mmoja wa Marekani kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kusema, mazungumzo kuhusu makubaliano hayo yataanza tena hivi karibuni katiika mji mkuu huo wa Austria.

Mikhail Ulyanov ameandika ujumbe kwenye ukurasa wa twitter kujibu madai ya Robert Malley, mwakilishi maalumu wa Marekani katika masuala ya Iran na kubainisha kwamba, mazungumzo ya Vienna yanayolenga kufufua tena JCPOA yataanza hivi karibuni; na inapasa pande husika katika makubaliano hayo zichukue hatua ya kutatua vizuizi vilivyosalia.

Mapema leo mwakilishi maalumu wa Marekani katika masuala ya Iran alikariri madai ya Washington dhidi ya Iran wakati alipohojiwa na jarida la Politico na kudai kwamba, hatima ya JCPOA iko mashakani.

Hadi sasa zimeshafanyika duru sita za mazungumzo huko mjini Vienna kwa madhumuni ya kuirejesha Marekani kwenye utekelezaji wa makubaliano hayo ya nyuklia, mazungumzo ambayo yamehudhuriwa na nchi zilizosalia katika JCPOA.

Mikhail Ulyanov

Iran imetamka bayana kuhusiana na suala hilo kwamba, sharti la kufikia mwafaka wa kuirejesha Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni kuhakikisha nchi hiyo inaondoa vikwazo vyote haramu na vya upande mmoja ilivyoiwekea Iran na kupata uthibitisho kwamba Washington imetekeleza hilo kivitendo.

Tarehe 8 Mei 2018 rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump alichukua hatua ya upande mmoja na ya kinyume cha sheria ya kujitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kuanza kutekeleza sera aliyoiita "mashinikizo ya juu kabisa" dhidi ya Iran.

Maafisa wa serikali ya sasa Marekani inayoongozwa na Joe Biden wamekiri kadhaa kuwa sera hiyo ya Trump imegonga mwamba na kudai kwamba wanataka kuirejesha Washington kwenye JCPOA; lakini hadi sasa wanakaidi kutekeleza hatua zinazohitajika ili kuweza kurejea katika makubaliano hayo.../

Tags