Nov 23, 2021 07:30 UTC
  • Ajali mbaya ya barabarani yaua watu 45 nchini Bulgaria

Makumi ya watu wameuawa katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea kusini mwa mji mkuu wa Bulgaria, Sofia.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchi hiyo, watu 45 wakiwemo watoto 12 wamepoteza maisha katika ajali hiyo ya leo Jumanne, iliyohusisha basi la abiria. 

Nikolay Nikolov, Mkuu wa Idara ya Zimamoto na Usalama wa Raia iliyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo amesema walioaga dunia katika ajali hiyo ni watu kati ya 45 na 46, na kwamba saba waliojeruhiwa wanatibiwa hospitalini.

Duru za habari zinaarifu kuwa, basi hilo lililohusika kwenye ajali hiyo lilikuwa likitokea Istanbul nchini Uturuki, likielekea mjini Skopje huko Macedonia Kaskazini.

Kiini cha ajali hiyo iliyotokea yapata kilomita 40 kusini mwa Sofia, mji mkuu wa nchi hiyo ya Ulaya hakijajulikana, lakini vyombo husika vimetangaza kuwa vimeanzisha uchunguzi.

Mabaki ya basi lililohusika na ajali Bulgaria

Septemba mwaka 2018, Mawaziri wa Usafiri, Ustawi na Mambo ya Ndani nchini Bulgaria, walijiuzulu nafasi zao wiki moja tangu kutokea ajali nyingine ya barabarani iliyosababisha vifo vya watu 17.

Kwa mujibu wa Kituo cha takwimu cha Umoja wa Ulaya, kumeshuhudiwa ongezeko kubwa la ajali za barabarani nchini Bulgaria katika miaka ya hivi karibuni, na hivyo kuifanya nchi hiyo kushika nafasi ya pili baada ya Romania, kwa kuwa na kiwango cha juu cha ajali za barabarani ikilinganishwa na nchi nyingine za umoja huo.

Tags